Michezo

Mashabiki wataka Migne atimuliwe kwa 'kuifeli' Stars

July 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

BAADHI ya washikadau wa soka katika eneo la Pwani, Jumanne walitaka Kocha wa Harambee Stars, Sebastien Migne ajiuzulu ama ang’atuliwe kutokana na matokeo mabaya kwenye dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Mwenyekiti wa Friends of Bandari FC, Ali Hassan Tito amesema kwamba lazima Migne ajiuzulu kwa hirai yake ama ang’atuliwe uongozini kwa sababu ameshindwa kutimiza ahadi ya kuunda kikosi imara kitakachoiletea sifa nchi.

“Inahuzunisha mkufunzi wa timu ya taifa kushindwa hata kupanga kikosi chake vizuri na kuacha wachezaji wengine wazuri nje ya kikosi hicho,” akasema Tito anayetaka mkufunzi huyo asihusishwe kuandaa kikosi cha timu itakayoshiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (CHAN) kwa wachezaji wa ligi ya nyumbani.

Akifafanua zaidi alisema kuwa inafahamika vizuri kuwa Francis Kahata ni mchezaji wa safu ya kiungo lakini anashangaa mechi zote amechezeshwa kama winga.

“Inaonyesha wazi kuwa Migne hajui namna ya kupanga timu yake,” akasema Tito.

Aidha, kinara huyo wa kikundi cha mashabiki wa Bandari alimlaumu vikali Migne kumchezesha kipa Patrick Matasi kwenye mechi zote ilhali katika mechi mbili zilizopita, alikuwa akifanya makosa hayo hayo.

“Hata kama alidaka penalti ya Sadio Mane na kuokoa mikwaju kadhaa, mabao aliyofungwa yalikuwa rahisi,” akasema Tito huku akidai kwamba kipa wa Bandari, Faruk Shikhalo amenyimwa haki ya kucheza hata angalau mechi moja kati ya tatu za Kundi C.

Uteuzi

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Admiral Youth FC, Aref Baghazally alidai kuwa uteuzi wa wachezaji haukufanyika kwa njia ya haki kwani uliwakosesha kiungo wa Bandari, Abdalla Hassan na winga Shaaban Kenga pamoja na Erick Ochieng wa Ulinzi Stars nafasi kuwa timuni.

“Inashangaza mno kuona Abdalla ambaye alikuwa mchezaji bora wa Januari na Kenga aliyeng’aa tangu mkondo wa pili uanze na Ochieng walicheza soka ya hali ya juu lakini kwa mshangao walinyimwa nafasi ya kucheza,” akalalama Baghazally.

Lakini Afisa Mkuu Mteule wa tawi la Pwani la Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Sumba Bwire amewapongeza wachezaji kwa kujitahidi ingawa walishindwa mechi mbili za Algeria na Senegal.

“Timu hizo mbili zina wanasoka wengi wanaocheza ligi za majuu,” akasema.

Bwire alitoa mfano wa timu ya Senegal kuwa kati ya kikosi chake cha wanasoka 23, kati yao 16 walikuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka uliopita hivyo hakuona ajabu kwa matokeo ya kushindwa.