• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mashabiki watarajiwa kufurika Kasarani gozi la ‘Mashemeji’

Mashabiki watarajiwa kufurika Kasarani gozi la ‘Mashemeji’

Na JOHN ASHIHUNDU

MASHABIKI watamiminika katika uwanja wa kimataifa wa Moi Kasarani leo Jumapili kushuhudia pambano kubwa kati AFC Leopards na watani wao wa tangu jadi Gor Mahia.

Ni mechi ambayo imekuja wakati timu zote zimefurahia matokeo mazuri mfululizo kwenye mechi zao tano zilizopita.

Katika mechi yao ya mwisho Gor Mahia ambao ndio mabingwa watetezi waliichapa Western Stima mabao 3-2, huku AFC Leopards wakiondoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chemelil Sugar, ugenini.

Gor Mahia wanashikilia nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 51, mbele ya Kakamega Homeboyz, kwa tofauti ya pointi nne, huku zikiwa zimesalia mechi 11.

AFC Leopards wako katika nafasi ya sita, kwa mwanya wa pointi 11 nyuma ya Gor, lakini hawajakata tamaa katika kampeni yao ya kutwaa ubingwa wa msimu huu. Vijana hao wa kocha Antony Kimani wamekuwa na mwelekeo mzuri tangu msimu huu uanze baada ya kusajili kipa Benjamin Ochan, raia wa Uganda ambaye anashirikiana vyema na mabeki wa kikosi hicho.

Ingwe, mabingwa wa taji hilo mara 13, wanatarajiwa kuvuruga matumaini ya K’Ogalo baada ya msimu uliopita kushindwa 4-1 katika mikondo yote miwili.

Leopards iliishinda Gor mara ya mwisho mnamo 2016, ugani Kasarani katika mechi ambayo ilimalizika kwa 1-0. Mara ya kwanza timu hizo zilipokutana mnamo 1968, Gor Mahia walichapwa 2-1.

Mara kwa mara timu hizi zinapokutana, pambano huwa linazua mihemko nchini Kenya, sawa na Yanga na Simba SC za Tanzania au Kaizer Chiefs na Orlando Pirates nchini Afrika kusini.

Mechi kati ya mahasidi hawa imepewa jina la Mashemeji Derby kutokana na uhusiano wa kijamii wa wafuasi wa timu hizo zenye ushawishi mkubwa nchini. Leopards itakuwa chini ya kocha Kimani ambaye mbinu zake zimeanza kuzaa matunda baada ya kuwa na vijana hao tangu Casa Mbungo aondoke mwishoni mwa mwaka uliopita.

Tayari Kimani amewakumbusha mashabiki kwamba lengo lake kubwa ni kuongoza Leopards kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu (KPL) ambao waliutwaa kwa mara ya mwisho mwaka 1998, timu hiyo ilipokuwa chini ya kocha Mtanzania, Sunday Kayuni.

Timu zote zitaingia uwanjani zikikabiliwa na hali ngumu ya kifedha kiasi cha kuanza kutafuta pesa kupitia kwa michango ya harambee.

Hapo awali, mara tu ligi hii ilipoanza, wachezaji wa timu hizi wamekuwa wakizuiwa kwenda mazoezi wakidai walipwe mishara na malimbikizi ya marupurupu yao. Leropards, ambao ndio wenyeji wa mechi ya kesho, wameandaa mipango kabambe ikiwemo kuweka ulinzi mkali kuhakikisha usalama umeimarishwa wakati wa mechi hiyo.

Kulingana na afisa mmoja wa Ingwe ambaye hakutaka kutajwa, wachezaji wote wako katika hali nzuri kuikabili vilivyo Gor Mahia.

Katika mechi ya leo, Leopards wanatarajiwa kutegemea huduma ya Elvis Rupia katika safu ya ushambuliaji kuvuruga ngome ya Gor Mahia ambayo ni dhaifu kwa sasa.

Tangua ajiunge na Ingwe mapema mwaka huu akitokea Power Dunamos ya Zambia ambaye zamani aliwahi kuchezea klabu za Nzoia Sugar na Wazito FC anajivunia jumla ya mabao tisa kufikia sasa.

Hata hivyo, kiungo mzuiaji Clyde Senaji ambaye majuzi alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi ambayoi Leopards ilishinda Chemelil kwa 1-0.

Lakini watamkaribisha nahodha, Robinson Kamura na Said Tsuma ambao hawakuwa kwenye mechi hiyo pamoja na Vincent Oburu ambaye amepata nafuu kutokana na jeraha, lakini Mervin Nabwire na Bonface Mukhekhe wanaendelea kuuguza majeraha.

  • Tags

You can share this post!

MWANAMKE MWELEDI: Amejiundia jina katika masuala ya...

RIZIKI: Hiki kinaweza kuyumba Mungu akakujalia kile

adminleo