Michezo

Mashetani Wekundu wazikwa na Everton

April 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

KLABU ya Everton Jumapili ilitanua mabawa yake dhidi ya mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Manchester United, pale ilipoichabanga 4-0 ugani Goodison Park.

Kichapo hicho sasa kimeyeyusha matumaini ya The Red Devils kutinga nne bora, siku chache tu baada ya kubanduliwa na Barcelona ya Uhispania kwenye robo fainali ya Klabu Bingwa Barani Ulaya(UEFA).

Man United walijipata nyuma mchezoni pale Richarlison de Andrade kumfunga David De Gea bao rahisi dakika ya 12 baada ya mechi kung’oa nanga . Glfyi Sigurdsson aliongeza bao la pili dakika 15, bao hili lilianika kudorora kwa fomu ya De Gea ambaye aliwahi kutajwa kama moja wa wanyakaji mahiri duniani.

Katika kipindi cha pili, vijana wa Marco Silva walirejea kwa matao ya juu na Lucas Digne akawapa bao safi baada ya safu ya ulinzi ya Manchester kulegea na kukosa kuondoa mpira kwenye eneo hatari.

Everton walitia msumari moto kwenye kidonda cha vijana wa Ole Gunnar Solskjaer pale winga wa zamani wa Arsenal Theo Walcott alipopokezwa krosi safi iliyomwacha moja kwa moja na De Gea na akafunga bao rahisi.

Baada ya kichapo hicho, Red Devils wamesalia katika nafasi ya sita, alama tatu nyuma ya nambari tatu Tottenham lakini mwanya huenda ukawa kubwa zaidi iwapo Arsenal na Chelsea zitashinda mechi zao dhidi ya Crystal Palace na Burnley mtawalia.

Nao vijana wa Unai Emery, Arsenal wameipa Man United matumiani ya kutinga nne-bora walipokubali kipigo cha 3-2 dhidi ya Crytal Palace uwanjani Emirates.