• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
Mashindano ya viziwi yaahirishwa

Mashindano ya viziwi yaahirishwa

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha kitaifa cha wanariadha wasio na uwezo wa kusikia (DAAK) kimelazimika kuratibu upya mashindano yaliyokuwa yafanyike humu nchini mwaka huu kutokana na virusi vya corona.

Ratiba mpya ya mbio hizo itatolewa rasmi wikendi hii baada ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kufichua tarehe mpya za kuandaliwa kwa makala ya nne ya riadha za kimataifa miongoni mwa watimkaji hao.

Awali, riadha za dunia kwa walemavu hao zilikuwa zimepangiwa kufanyika kati ya Julai 18-25 mjini Radom, Poland. Hata hivyo, maandalizi yalisitishwa kwa hofu ya kusambaa zaidi kwa maambukizi ya homa kali ya virusi vya corona.

Afisa wa Mawasiliano wa DAAK, Tom Okiki, amesema wasimamizi wa riadha hizo kwa sasa wanashauriana na washikadau wote kabla ya kuafikiana kuhusu tarehe mpya.

Hadi kufanyika kwa riadha hizo za dunia, watimkaji wa Kenya walikuwa wamepangiwa kushiriki mashindano matatu ya kujifua ambayo kwa sasa yamefutiliwa mbali.

Mojawapo ya mbio hizo ni makala ya saba ya Deaf Half Marathon yaliyokuwa yafanyike mjini Nakuru mnamo Aprili 26 kisha makala ya tatu tano ya National Deaf Track na Field Championships yaliyokuwa yaandaliwe uwanjani MISC Kasarani, Nairobi kati ya Mei 29-30, 2020.

Baada ya hapo, kikosi cha mwisho ambacho kingeteuliwa kuwakilisha Kenya nchini Poland kingeshiriki mbio za kitaifa za nyika mnamo Juni 7 katika uwanja wa Uhuru Gardens, Nairobi.

Baadaye, kikosi kingepiga kambi kwa mazoezi ya wiki mbili ugani Kasarani kati ya Juni 29 na Julai 13 kisha kufunga safari ya kuelekea Poland.

“Tulipanga kutumia mashindano hayo ya ndani kwa ndani kujiandalia kwa makala ya nne riadha za dunia. Sasa tutalazimika kuratibu upya mbio hizo baada ya IAAF kutoa kalenda nyingine,” akasema Okiki.

Wengi wa wanariadha wa humu nchini wasio na uwezo wa kusikia wamekuwa wakishiriki mazoezi kivyao katika maeneo tofauti kwa matumaini ya kutia fora katika mchujo na hatimaye kupata fursa ya kuwakilisha Kenya nchini Poland.

Samuel Kibet ambaye ni kocha wa timu ya taifa ya Kenya amewataka wanariadha wote wanaojiandaa kwa mashindano hayo ya kimataifa kutolegeza kamba mazoezini.

“Kuahirishwa kwa mbio hizo ni nafuu zaidi kwa wanariadha wetu ambao kwa sasa wana muda maridhawa wa kujizatiti vilivyo,” akasema Kibet.

DAAK inatazamia kuwa na wanariadha watakaowakilisha Kenya katika fani 16 tofauti nchini Poland.

Kwingineko, shughuli za ukarabati wa uwanja wa Kasarani uliokuwa uwe mwenyeji wa mbio za Continental Tour na riadha za dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka huu bado zinaendelea licha ya mashindano hayo kuahirishwa.

Haya ni kwa mujibu wa Waziri wa Michezo, Amina Mohammed, ambaye amesisitiza kuwa bado wanasubiri kutoka kwa IAAF kuhusu tarehe ya kuandaliwa upya kwa mbio hizo ambazo hapo awali, zilikuwa zifanyike kati ya Julai 7-12, 2020.

Maamuzi ya kuahirishwa kwa mashindano hayo yaliafikiwa baada ya mashauriano ya kina na wahusika mbalimbali, pamoja na mashirikisho wanachama yaliyokuwa yashiriki riadha hizo.

Matabibu wa IAAF wanaoshirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), wanashikilia kwamba viwango vya kuenea kwa homa ya corona miongoni mwa mataifa mbalimbali ulimwenguni ni vya kutisha mno kwa sasa, na mojawapo ya njia kuu za maambukizi ni mikusanyiko ya umma.

Amina pia amepongeza hatua ya IAAF na serikali ya Japan kuahirisha Olimpiki za Tokyo 2020. Riadha nyinginezo za dunia ambazo tayari zimeahirishwa ni ile ya Indoor Championships mjini Nanjing, China; Nusu Marathon ya Dunia mjini Gdynia, Poland na Matembezi yaliyokuwa yaandaliwe mjini Minsk, Belarus.

Nchini Kenya, mamia ya wanariadha tayari wamesimamisha mazoezi katika zaidi ya kambi 30 za mazoezi zilizoko Kaunti za Nandi na Elgeyo Marakwet kutokana na virusi vya corona.

  • Tags

You can share this post!

‘Msiwakate mshahara wafanyakazi wa Tottenham’

Ratiba za Riadha za Dunia na Jumuiya ya Madola zagongana

adminleo