Mataifa 16 kushiriki katika michuano ya CHAN 2020
Na JOHN ASHIHUNDU
WALIOKUWA wachezaji tegemeo wa timu ya taifa ya Cameroon, Salomon Olembe na Stephen Tataw ni miongoni mwa watu mashuhuri walioendesha shughuli za droo ya michuano ya CHAN 2020 itakayojumuisha mataifa 16.
Wengine walioendesha shughuli hiyo ya Jumatatu katika ukumbi wa Palais Polyvament de Sport De Younde, ni pamoja na Mkurugenzi wa Mashindano katika Shirikisho la Kandanda Afrika (CAF), Samson Adamu.
Fainali hizo za wachezaji wanaoshiriki katika ligi za nyumbani itafanyika kati ya Aprili 4 na Aprili 25 katika miji ya Yaounde, Douala na Limbe.
Wakati wa droo hizo, kadhalika atakuwepo Rais wa CAF, Ahmad Ahmad, Waziri wa Michezo na Elimu ya Mazoezi ya Viungo nchini Cameroon, Narcisse Moulle Kombi pamoja na wanachama wa kamati andalizi ya kitaifa ya CHAN 2020.
Tataw anafahamika kuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi kuwahi kuchezea timu ya Cameoon, hasa alipokuwa nahodha wa kikosi kilichotinga robo-fainali ya fainali za Kombe la Dunia mnamo 1990 nchini Italia.
Kadhalika, alikuwa nahodha wa timu ya Cameroon iliyotwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mnamo 1988 nchini Morocco, lakini kwa sasa ni mfanyakazi katika idara ya kiufundi ya Shirikisho la Soka Cameroon (Fecafoot)
Kwa upande mwingine, Olembe aliichezea Cameroon mara 60 kati ya 1997 na 2007. Alikuwa katika kikosi kilichoshiriki katika fainali za Kombe la Dunia nchini Ufaransa mnamo 1998 na Japan mnamo 2002.
Alikuwa kwenye kikosi cha Nantes kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (French Ligue 1) mnamo 2001 kabla ya kuchezea Olympique Marseille ya Ufaransa, halafu Leeds United na Wigan nchini Uingereza miongoni mwa timu zingine kabla ya kustaafu mwaka 2010. Kwa sasa ndiye meneja wa timu ya taifa maarufu kama Indomitable Lions.
Mbali na wenyeji Cameroon, timu zingine zitakazoshiriki michuano ya CHAN ni Congo, DR Congo, Rwanda, Uganda na Tanzania, Morocco, Libya, Namibia, Zambia, Zimbabwe, Guinea, Mali, Burkina Faso, Niger na Togo.
Droo kamili ni kama ifuatavyo:
Kundi A
Cameroon
Mali
Burkina Faso
Zimbabwe
Kundi B
Libya
Congo DR
Congo
Niger
Kundi C
Morocco
Rwanda
Uganda
Togo
Kundi D
Zambia
Guinea
Namibia
Tanzania