• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Matic kuchezea United hadi 2023

Matic kuchezea United hadi 2023

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO Nemanja Matic, 31, amerefusha kandarasi yake kambini mwa Manchester United hadi Juni 2023.

Nyota huyo mzawa wa Serbia alisajiliwa kutoka Chelsea mnamo 2017 na mkataba wake wa awali uwanjani Old Trafford ulitarajiwa kutamatika rasmi mnamo Juni 2021.

“Kama mchezaji, nahisi kwamba bado nina malengo mengi ambayo nina uwezo wa kuyaafikia kitaaluma. Kufaulisha mipango yote hiyo nikivalia jezi za Man-United kutanipa fahari tele,” akatanguliza Matic.

“Kuhusishwa na Man-United ni tija kwa mwanasoka yeyote. Upekee wa kikosi hiki ni mseto mzuri wa chipukizi na wanasoka wazoefu,” akangeza.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer amesema “anafurahishwa sana” na hatua ya Matic kutia saini mkataba mpya na kusisitiza kwamba tajriba, utaalamu na uongozi wa kiungo huyo utachangia pakubwa kuimarisha makali ya kundi la wanasoka wake chipukizi.

Kufikia sasa, Matic amewajibishwa na Man-United katika jumla ya michuano 27 msimu huu. Chini ya Solskjaer, Man-United hawajapoteza mechi yoyote kati ya 16 zilizopita katika mapambano yote tangu Januari 2020.

Matic anarefusha mkataba wake uwanjani Old Trafford  baada ya kiungo Scott McTominay kutia saini kandarasi mpya hadi Juni 2025.

Kurefushwa kwa kandarasi ya McTominay mwenye umri wa miaka 23 ni zao la kuimarika kwa kiwango cha makali yake tangu awajibishwe kwa mara ya kwanza na kocha wa zamani Jose Mourinho dhidi ya Arsenal mnamo Mei 2017.

Chipukizi huyo aliyeanza kupokezwa malezi ya soka akiwa katika akademia ya Man-United, kwa sasa anajivunia kuchezeshwa na waajiri wake katika jumla ya michuano 75 ambapo amefunga mabao sita katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

You can share this post!

Magari ya uchukuzi wa umma yatakiwa kuwa na kibali maalum

Polisi kizimbani kwa kumumunya mamilioni ya NSSF

adminleo