Mauritania wapata ushindi wa kwanza unaowaponyoka Tanzania katika AFCON
NA LABAAN SHABAAN
Mabingwa mara mbili wa Kinyang’anyiro cha Kandanda Afrika (AFCON) Algeria walibanduliwa nje ya shindano Jumanne baada ya kuchapwa na Mauritania bao moja kwa nunge.
Jeneza la Algeria liligongomelewa msumari mmoja na wa mwisho dakika ya 37 baada ya nahodha Mohamed Yaly kutikisa nyavu na kuchacharusha mashabiki.
Kocha wa Algeria Djamel Belmadi alibaki kinywa wazi baada ya kushindwa kwa uchungu.
“Kuna mambo siwezi kueleza; hatujaweza kufunga licha ya kuwa na mpango na mbinu nzuri,” akasema.
Matokeo haya yamefungulia Mauritania ukurasa mpya wa kushiriki mkondo wa timu 16 wa mashindano yanayoendelea nchini Ivory Coast.
Ni ushindi wao wa kwanza wa AFCON ambao hakika umeandikwa katika buku la historia ya taifa hilo linaloonekana dhaifu kutamba katika dimba hili.
Kabla ya mechi, Mkufunzi wa Mauritania Amir Abdou aliwaambia vijana wake: “Mna nafasi ya kunakili historia dhidi ya Algeria.”
Hatimaye hii ilitimia wakiwa na umiliki finyu wa asilimia 25 wa mchezo dhidi ya waarabu wa Afrika.
Kocha Abdou amekuwa wembe unaokata miti mikuu ikikumbukwa masaibu aliyowalimbikizia Ghana katika makala ya AFCON ya 2021.
Wakati huo Amir alifunza Comoros ambao waliwapiku Ghana na kuwatimua nje ya kinyang’anyiro.
Na sasa ameangusha miamba wa Afrika wenye uzoefu wa kushiriki mashindano haya.
Sawa na Mauritania, Taifa Stars wa Tanzania wana nafasi ya kuandika historia wakidunda uwanjani dhidi ya Ingwee wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo Jumatano saa tano usiku.
Simba wa Chinguetti walifuzu katika nafasi ya tatu na pointi tatu nyuma ya Burkina Faso na Angola kundini D.