Maveterani wa Man City wala sare gozi la Kompany
Na MASHIRIKA
ULIKUWA usiku wa kufana kwa Vincent Kompany uwanjani Etihad baada ya mechi ya kumsherehekea kati ya vigogo wa Manchester City (Man City Legends) na wale Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League All-Stars) kutamatika 2-2.
Kompany mwenyewe hakushiriki kutokana na jeraha la mguu, akitaniana kabla ya mechi kuwa ilimfaa zaidi kuwa shabiki akiwa mkekani.
Hata hivyo, ilikuwa burudani tosha kwa shujaa huyo Mbelgiji, ambaye alihama City mwisho wa msimu uliopita baada ya kuichezea miaka 11 iliyosheheni mataji, mbele ya mashabiki 51,602.
Huku mechi ya City ya Ligi Kuu dhidi ya Norwich ikinukia kesho usiku, kocha wa Man City Legends Pep Guardiola alichezesha David Silva na Sergio Aguero nusu saa pekee.
Mshambuliaji wa zamani wa City, Mario Balotelli alihudhuria mechi hiyo, ingawa hakucheza.
Sababu ya Balo, ambaye alivalia jezi ya City kati ya mwaka 2010 na 2013, kutocheza pengine ni kuwa hakuwa amefahamisha waajiri wake Brescia alikokuwa, huku akitarajiwa kurejea mazoezini mapema Alhamisi.
Bao la mapema
Timu ya Man City Legends ilianza mechi vyema ilipoona lango katika dakika ya pili baada ya Martin Petrov kumpita Gary Neville kama risasi pembeni kushoto kabla ya winga huyo wa zamani wa City kumwaga kipa Edwin van der Sar.
Bao hilo la mapema lilizua ubishi mkali kati ya Neville na beki mwenza Jamie Carragher kuhusu nani kati yao alistahili kulaumiwa kwa kulibababisha, ingawa mwishowe Neville alikubali lawama.
Nyota wa zamani wa Manchester United na Uingereza Paul Scholes alisakatia All-Stars mechi nzima, miaka sita baada ya kuangika daluga zake uwanjani Old Trafford. Hata hivyo, Scholes, 44, alionyesha bado yuko fiti.
Nduguye Vincent, Francois Kompany aliingizwa kama mchezaji wa akiba katika kipindi cha pili. Mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 29 ni beki wa pembeni kushoto katika timu ya pili ya klabu ya Roeselare inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ubelgiji. Vincent alisema kuwa sikitiko lake ni kuwa hakuweza kushirikiana na Francois uwanjani katika mechi hiyo.
Naye Neville kwa bahati mbaya alicheza dakika 35 pekee. Beki huyo wa pembeni kulia alipumzishwa alipoumia akijaribu kumkimbiza Craig Bellamy dakika chache baada ya Robbie Keane kukamilisha kwa ustadi shambulio tamu lililofanywa na Robin van Persie na Ryan Giggs.
Van Persie kisha aliweka All-Stars mabao 2-1 mbele dakika ya 48 baada ya Tim Cahill kumega pasi murwa kupitia kisigino.
Benjani Mwaruwari alisawazishia Man City Legends sekunde chache kabla ya refa Mark Halsey kupuliza kipenga cha mwisho kupitia ikabu kutoka kwa Nigel de Jong.
Bada ya mechi, Vincent Kompany alishukuru mashabiki kwa kutambua ufanisi wake pamoja na kusaidia katika uchangishaji wa fedha za kutafutia watu wasio na makao mjini Manchester mahali pa kuishi.
Fedha zote zitakazokusanywa kutoka mechi hiyo zitatolewa kwa shirika la kutoa misaada la Tackle4MCR, ambalo lengo lake ni kumaliza tatizo la watu kuishi mitaani mjini Manchester.