MAVIZIONI: Arsenal kucheza dhidi ya Bournemouth
Na MASHIRIKA
BOURNEMOUTH, Uingereza
WASHINDI wa mataji mengi ya Kombe la FA, Arsenal watalenga kujiunga na wenzao kutoka Ligi Kuu (EPL) Chelsea, Leicester, Sheffield United na Norwich katika raundi ya 16-bora, watakapovizia Bournemouth leo Jumatatu usiku.
Chelsea ilijikatia tiketi kwa kulemea wenyeji Hull 2-1 kupitia mabao ya Michy Batshuayi na Fikayo Tomori.
Kelechi Iheanacho alifungia Leicester bao la pekee ikichapa Brentford 1-0.
Norwich walizima Burnley 2-1 nayo Sheffield United ikalemea Millwall 2-0 Jumamosi.
West Ham iliaga kombe baada ya kuchabangwa na West Brom 1-0 uwanjani London, licha ya wapinzani wao wa kutoka Ligi ya Daraja ya Pili kumaliza mechi watu 10.
Southampton na Tottenham zitarudiana ili kuamua atakayesonga mbele baada ya kutoka 1-1 uwanjani St Mary’s. Newcastle na Oxford pia zitarudiana baada ya kutoka 0-0 uwanjani St James’ Park.
Itakuwa mara ya kwanza kabisa Bournemouth na Arsenal kukutana kwenye kombe hili.
Mabingwa mara 13 Arsenal, ambao walishinda kombe hili mara ya mwisho msimu 2016-2017, wana rekodi nzuri dhidi ya Bournemouth.
Vijana hao wa kocha Mikel Arteta watashuka ugani Vitality wakijivunia kutoshindwa na Bournemouth katika mechi 10 kati ya 11 ambazo wamekutana.
Safari zote nne zilizopita za Arsenal uwanjani Vitality zimeishia kwa kila timu kupata bao, ikiwemo mara ya mwisho Desemba 26 mwaka jana zilipotoka 1-1.
Mmoja wa wachezaji wanaotarajiwa kuongoza mashambulizi ya Arsenal ni Gabriel Martinelli.
Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 18 amekuwa akifanyia ‘wanabunduki’ kazi nzuri. Alifikisha mabao 10 msimu huu alipoona lango dhidi ya Chelsea timu hizo zikitoka sare ya 2-2 Jumanne iliyopita.
Pierre-Emerick Aubameyang atakosa mchuano huu. Mgabon huyo atakuwa akimaliza marufuku yake ya mechi tatu. Beki David Luiz pia yuko nje baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Chelsea.
Bournemouth ya kocha Eddie Howe ilichapa Luton Town 4-0 katika raundi iliyopita, na kumaliza mikosi ya kutoshinda mechi kwenye kipute hiki tangu Januari 2016.
Vijana wa Howe, ambao hawajapita raundi ya 32-bora tangu 1989, wanashikilia nafasi ya 18 kwenye Ligi Kuu (EPL).
Mashambulizi yao yanatarajiwa kuongozwa na Callum Wilson. Arsenal, ambao walibandua nje Leeds katika raundi iliyopita, wako katika nafasi ya 10.
Mabingwa watetezi Manchester City waliratibiwa kumenyana na Fulham, Liverpool ilimane na Shrewsbury nayo Manchester United ivaane na Tranmere baadaye jana.
Matokeo ya raundi ya tano (Januari 25): Southampton 1-1 Tottenham, Burnley 1-2 Norwich, Brentford 0-1 Leicester, Portsmouth 4-2 Barnsley, Coventry 0-0 Birmingham, West Ham 0-1 West Brom, Hull City 1-2 Chelsea, Reading 1-1 Cardiff City, Millwall 0-2 Sheffield United, Newcastle 0-0 Oxford.