Michezo

Mawakala wa Ozil sasa kutua nchini Amerika kufanikisha uhamisho wake hadi DC United

August 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

VINARA wa kikosi cha DC United nchini Amerika wamemtaka kiungo Mesut Ozil kukubali mshahara mdogo ili ajiunge na miamba hao wa Major League Soccer (MLS) wanaopania kulijaza pengo la Wayne Rooney.

Ozil kwa sasa ndiye mchezaji wa pili baada ya Alexis Sanchez wa Manchester United anayedumishwa kwa mshahara wa juu zaidi katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Nyota huyu wa zamani wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ujerumani kwa sasa hutia mfukoni kima cha Sh46 milioni kwa wiki. Ukubwa wa gharama ya kumdumisha Ozil uwanjani Emirates ni kiini cha usimamizi wa Arsenal kutaka kuagana naye, na tayari mawakala wake wamefichua kuhusu mpango wa kutua jijini Washington kuanzisha mazungumzo na DC United kuhusu uwezekano wa kumsajili.

Kiini cha DC United kuyahemea maarifa ya Ozil ni kujaza nafasi ya Rooney ambaye kwa sasa anajiandaa kuanza majukumu ya kuwa kocha na mchezaji wa Derby County mnamo Januari 2020.

Hata hivyo, huenda fedha zikawa kikwazo kikubwa katika jitihada za Ozil kubanduka kambini mwa Arsenal ambao watalazimika kugharimia sehemu kubwa ya mshahara wa nyota huyu.

Tayari Kuondoka kwa Rooney kambini mwa DC United ni afueni kubwa kwa kikosi hicho ambacho kimekuwa kikimpokeza mshahara wa hadi Sh11 milioni kwa wiki.

Kwa sasa, ina maana kwamba Ozil anapokezwa mshahara ambao ni mara tatu zaidi kuliko ule ambao mchezaji ghali zaidi katika MLS hutia kapuni mwishoni mwa kila wiki.

Mshahara wa Ibrahimovic

Mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic ambaye ndiye sogora ghali zaidi katika ligi hiyo, hutia kapuni kiasi cha Sh15 milioni kwa wiki kambini mwa LA Galaxy.

Iwapo mwafaka hautapatikana kati ya Arsenal na DC United, basi huenda Ozil akajipata akisalia kusugua benchi zaidi ugani Emirates chini ya kocha Unai Emery ambaye kwa sasa anajivunia huduma za sajili ghali zaidi Nicolas Pepe na kiungo Dani Ceballos aliyetokea Real Madrid kwa mkopo.

Ozil alikosa sehemu kubwa ya kampeni za Arsenal msimu jana kutokana na wingi wa visa vya mejaraha, huku kiwango cha kujituma kwake kila alipopangwa kikosini kikitiliwa shaka na kocha Emery.

Kwa pamoja na Alexandre Lacazette na Sead Kolasinac, sogora huyu mzawa wa Uturuki na raia wa Ujerumani hakuwa sehemu ya kikosi cha Arsenal kilichochuana na Newcastle United wikendi jana.

Mvamizi Pierre-Emerick Aubameyang aliwafungia Arsenal bao la pekee na la ushindi katika mechi hiyo ya EPL dhidi ya Newcastle United ugani St James’ Park. Chini ya Emery, Arsenal walianza mchuano huo wakiwa na sajili wao wapya waliogharimu zaidi ya Sh16 bilioni muhula huu kwenye benchi.