Mbappe awaambia PSG anataka kuagana nao mwishoni mwa msimu wa 2020-21
Na MASHIRIKA
KYLIAN Mbappe, 21, amewaarifu Paris Saint-Germain (PSG) kuhusu matamanio yake ya kuagana nao mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21 ili ajiendeleze zaidi kitaaluma kwingineko.
Akiwa shabiki sugu wa Liverpool, Mbappe anapigiwa upatu wa kutua Uingereza kuvalia jezi za miamba hao wa Ligi Kuu ya EPL au kuyoyomea Uhispania kuchezea Real Madrid ambao wamekuwa wakimvizia kwa muda mrefu uliopita.
Mbappe alisajiliwa na PSG kutoka AS Monaco mnamo 2018 kwa kima cha Sh23 bilioni. Usajili wake ndio ghali zaidi kwa chipukizi na unasalia kuwa wa pili ulio ghali zaidi katika historia ya soka baada ya ule wa Sh28 bilioni uliomshuhudia fowadi Neymar Jr akimbanduka kambini mwa Barcelona na kutua PSG mnamo 2017.
Mbappe ambaye pia amekuwa akihusishwa na Manchester City kwa kipindi kirefu, alitia saini kandarasi ya miaka mitano na PSG mnamo 2018.
Mbappe ambaye ni mzawa wa Ufaransa, aliwafungia PSG jumla ya mabao 29 kutokana na mechi 33 za msimu wa 2019-20.
Waingereza Raheem Sterling, Jadon Sancho, Trent Alexander-Arnold na Marcus Rashford ni miongoni mwa chipukizi watano wa thamani ya juu zaidi kwa sasa katika soka ya bara Ulaya.
Orodha hiyo inaongozwa na Mbappe ambaye thamani yake inakadiriwa sasa kufikia Sh32.3 bilioni.
Orodha hiyo iliyoandaliwa na shirika la CIES Football Observatory iliwalenga wanasoka wanaoshiriki Ligi Kuu tano za soka ya bara Ulaya, yaani Uingereza (EPL), Ujerumani (Bundesliga), Uhispania (La Liga), Ufaransa (Ligue 1) na Italia (Serie A).
Sterling, 25, ameingia katika orodha ya wanasoka wa haiba kubwa zaidi kambini mwa Man-City na timu ya taifa ya Uingereza tangu abanduke uwanjani Anfield alikokuwa akivalia jezi za Liverpool mnamo 2015.
Fowadi huyo anayemezewa mate na Real Madrid ya Uhispania anashikilia nafasi ya pili miongoni mwa wachezaji walio na thamani kubwa zaidi ulimwenguni (Sh24 bilioni) mbele ya Sancho (Sh22 bilioni).
Huduma za Sancho ambaye kwa sasa ni kiungo wa Borussia Dortmund nchini Ujerumani, zinahemewa pakubwa na Manchester United na Man-City.
Alexander-Arnold wa Liverpool, 21, anashikilia nafasi ya nne (Sh21 bilioni) mbele ya Rashford (Sh19 bilioni) ambaye amefungia Man-United jumla ya mabao 14 kutokana na mechi 22 za EPL msimu huu.
Miongoni mwa masuala yaliyozingatiwa na CIES katika kujumuisha orodha ya wanasoka hao wa thamani kubwa zaidi duniani ni umri wao, matokeo yao katika ngazi za klabu na timu ya taifa na mfumo wa sasa wa usajili katika soko la uhamisho wa wachezaji.