Michezo

Mbunge agawia vijana vifaa vya michezo ili watumie vizuri likizo ndefu ya Disemba

Na OSBORN MANYENGO November 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

ZAIDI ya klabu 15 za soka na voliboli kutoka eneo bunge la Saboti, Kaunti ya Trans-Nzoia zilipokea msaada wa vifaa vya michezo kutoka kwa mbunge wa eneo hilo, Caleb Amisi.

Akipokeza klabu hizo mpira na vifaa vingine vya spoti, mbunge huyo alisema lengo kuu ni kuona vijana wengi wakishiriki michezo wakati huu wa likizo ndefu ya Disemba baada ya kufunga shule ili kuendeleza talanta zao.

Klabu hizo zikiwemo 12 za soka na tatu za voliboli zilipokea mipira na vifaa vingine, huku Transfoc FC inayoshiriki ligi ya Taifa Daraja la Kwanza zoni B ikiwa miongoni mwa timu kongwe zilizonufaika kutokana na msaada huo.

Klabu zikipokea vifaa vya michezo kutoka kwa Mbunge wa Saboti Caleb Amisi. Picha|Osborn Manyengo

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya timu, katibu wa timu hiyo, Pascal Wekesa alisema msaada huo utawasaidia sana akisema wamekuwa wakihangaika kupata vifaa vya michezo ikiwamo mpira wa kufanyia mazoezi, huku akimpongeza mbunge huyo na kutoa wito kwa wahisani wengine kuiga mfano wake na kufadhili ukuzaji wa talanta mashinani.