Michezo

Mbuzi Hennes IX wa FC Cologne apigwa marufuku uwanjani kwa mara ya kwanza baada ya miaka 12

May 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA

MBUZI maarufu ambaye amekuwa akitumiwa na kikosi cha Cologne kama maskoti kwa kipindi kirefu, sasa amepigwa marufuku ya kuingizwa uwanjani kwa mara ya kwanza baada ya miaka 12 kutokana na kanuni mpya za afya.

Cologne ambao hushiriki Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) wamekuwa na maskoti ya mbuzi aitwaye Hennes katika mechi zao zote za nyumbani tangu 1950. Mbuzi huyo amekosekana katika mchuano mmoja pekee mnamo 2008 baada ya kuugua ghafla.

Hennes wa Tisa, ambaye huu ni msimu wake wa kwanza akiwa maskoti wa Cologne, amekuwa na watangulizi wanane tangu kikosi hicho kianze kutumia maskoti za mbuzi yapata miaka 70 iliyopita.

Ingawa hivyo, kutokana na kanuni mpya ambazo waendeshaji wa Ligi za soka za Ujerumani (DFL) wanastahili kuzingatia ili kudhibiti janga la corona, Hennes atalazimika kusalia nje ya uwnaja kwa muda.

Kwa sasa atawekwa katika hifadhi ya wanyama ya Kolner Zoo hadi pale sheria zinazoongoza kipute cha Bundesliga kwa sasa zitakapolegezwa.

Kwa sasa, ni watu 322 pekee wanaokubaliwa ndani ya uwanja wakati wa mechi za Bundesliga huku wachezaji pia wakidhibitiwa na msharti makali.

Hivyo, maskoti zote katika soka ya Ujerumani kwa sasa zimepigwa marufuku kwa muda usiojulikana.

“Kuzingiatia kanuni za afya katika kiwango cha mtu binafsi ndilo jambo muhimu zaidi katika juhudi za kuzuia maambukizi ya corona,” ikasema sehemu ya taarifa ya DFL.

Ina maana kwamba tai aitwaye Attila ambaye amekuwa akitumiwa na kikosi cha Eintracht Frankfurt kama maskoti, pia hatakuwa ugani wakati wa mechi zote za nyumbani za kikosi hicho kilichorejelea kampeni za Bundesliga msimu huu dhidi ya Borussia Monchengladbach mnamo Mei 16, 2020.

Ndege huyo amekuwa sehemu ya historia ndefu ya kikosi cha Frankfurt huku mitindo ya kupaa kwake kwenye anga za uwanja ikiwa miongoni mwa mambo yanayochochea mashabiki wengi kuhudhuria mechi za nyumbani za klabu hiyo.

Mechi za Bundesliga zilirejelewa Mei 16 huku Cologne almaarufu ‘Billy Goats’ wakitazamiwa kushuka dimbani kuvaana na Mainz katika uga wao wa nyumbani wa Rhein-Energie mnamo Mei 17, 2020.

Cologne wamekuwa na maskoti ya mbuzi tangu 1950 na mnyama huyo alipagazwa jina Hennes na mmojawapo wa maafisa wa klabu hiyo kwa heshima ya aliyekuwa kocha wao wakati huo, Hennes Weisweller.

Hennes wa Tisa alianza kutekeleza majukumu yake kambini mwa Cologne msimu huu baada ya mtangulizi wake, Hennes wa Nane, kustaafishwa kutokana na matatizo ya afya yasababishwayo na umri wa mkubwa.

“Tusingependa kabisa kuona Hennes akitatizika kusimama au kutembea ugani kutokana na maumivu ya mifupa na viungo. Baada ya Cologne kupandishwa ngazi hadi Bundesliga na msimu huu kutamatika rasmi, sasa ni wakati mwafaka kwa Hennes wa Nane kustaafu,” akasema mkurugenzi msimamizi wa Cologne, Alexander Wehrle mwishoni mwa msimu uliopita.