Michezo

Mbwa mwitu na Man Utd kugongana tena taji la FA

January 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

WOLVERHAMPTON, Uingereza

MANCHESTER United na Wolverhampton Wanderers zitakutana tena baada ya mechi yao ya FA Cup kumalizika kwa sare ya kutofungana ugani Molineux, siku ya Jumamosi usiku.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa vijana hao wa kocha Ole Gunnar Solskjaer kushindwa kuwika katika mashindano hayo tangu 2015, wakati huu wakijiandaa kucheza na Manchester City katika mikondo miwili ya nusu-fainali ya mechi za EFL Cup.

Ugani Molineux, makombora ya Marcus Rashford na Raul Jimenez wa Wolves katika kipindi cha pili yaligonga mwamba na kutoka nje.

Kadhalika Rashford alikaribia kufunga mara tu alipoingizwa uwanjani katika kipindi cha pili kombora lake lilipomchanganya nahodha Conor Coady.

Jimenez atajilaumu mwenyewe kwa kushindwa kufunga bao baada ya kubakia yeye tu na kipa Sergio Romero.

Wolves, ambao msimu wao ulianza Julai, walimpa nafasi kinda mshambuliaji Benny Ashley-Sela.

Kinda huyu alionyesha kiwango cha juu cha mchezo kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Jimenez baada ya kipindi cha mapumziko.

Wolves walipoteza nafasi ya wazi mapema katika mechi hiyo, baada ya kona ya Pedro Neto kumpata Matt Doherty karibu na lango, kabla ya Romero kuokoa kwa kishindo.

Baadaye, Romero alimpokonya Neto mpira miguuni baada ya Mreno huyo kupata pasi kutoka kwa Adam Traore katika eneo la hatari.

Mpira wa fri-kiki wa Juan Mata ulikosea tu kidogo kujaa wavuni, kabla ya Rashford kupiga mlingoti zikibakia dakika 19 mechi kumalizika, hata kabla ya kipa John Ruddy kufanya juhudi zozote za kuzuia hatari.

Kumbukumbu 2006

United walichezea Molineux kwa mara ya mwisho mnamo 2006, wakati huo wakiwa chini ya Sir Alex Ferguson ambapo waliibuka na ushindi wa 3-0, katika raundi ya nne ya michuano hii.

Kikosi cha Ferguson siku hiyo kilikuwa na nyota kadhaa wakiwemo Wayne Rooney na Ruud van Nistelrooy, ambao ni miongoni mwa majagina wa soka.

Kwa sasa kikosi hiki cha kocha Ole Gunnar hakina mastaa wa kutegemea kama ilivyokuwa nyakati za Ferguson, hasa baada ya Rashford kuanza kama mchezaji wa akiba, huku Anthony Martial akikosena kutokana na maradhi ya ghafla.

Ilikuwa mechi ngumu kwa Manchester United ambao walishindwa kabisa kuwika mbele ya vijana hao matata wa Wolves.

Timu hizo ambazo tayari zimetinga raundi ya 32 ya michuano ya Europa League zitarudiana ugani Old Trafford.

Wolves hawajashindwa na Manchester United katika mechi tano za karibuni tangu msimu wa 1959-1962.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa vigogo hao kushindwa kufunga bao langoni mwa Wolves baada ya kukutana mara 14 katika mashindano yote, tangu washindwe 1-0 na Wolves katika pambano la EPL mnamo 2004.