Mbwana Samatta ajiunga na Fenerbahce kwa mkopo akitoka Aston Villa
Na MASHIRIKA
FOWADI matata raia wa Tanzania, Mbwana Samatta, 27, amejiunga na Fenerbahce ya Ligi Kuu ya Uturuki kwa mkopo kutoka Aston Villa ya Uingereza.
Fenerbahce wamefichua kwamba watampa nyota huyo mkataba wa kudumu wa miaka minne mwishoni mwa msimu huu.
Samatta alijiunga na Villa mnamo Januari 2020 baada ya kuagana rasmi na kikosi cha Genk cha nchini Ubelgiji.
“Nashukuru Villa kwa kunipa fursa ya kutimiza ndoto yangu ya tangu utotoni ya kunogesha gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL),” akasema Samatta.
Akiwa Uingereza, Samatta alifunga bao lake la kwanza la EPL dhidi ya Bournemouth katika mechi ya kwanza ndani ya jezi za Villa kisha akafunga la pili kwenye fainali ya Carabao Cup iliyowakutanisha na Manchester City uwanjani Wembley mnamo Machi 2020.
Hayo ndiyo mabao ya pekee ambayo Samatta alifungia Villa katika kipindi kizima cha kuhudumu kwake ugani Villa Park.
Kisu cha makali ya sogora huyo kilisenea pakubwa tangu kurejelewa kwa mech za EPL mnamo Juni 2020 baada ya mkurupuko wa virusi vya corona.
Samatta aliachwa nje ya kikosi cha Villa kilichowalaza Sheffield United 1-0 katika mechi ya kwanza ya EPL msimu huu wa 2020-21 mnamo Septemba 21, 2020.
Villa waliibuka na ushindi wa 1-0 katika mechi hiyo iliyochezewa Villa Park.
Samatta amewahi pia kucheza Simba SC ya Tanzania (2010-11) kabla ya kuyoyomea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) kuvalia jezi za TB Mazembe kati ya 2011 na 2016.
Alichezea Genk kwa muda wa miaka minne (2016-20) kabla ya kusajiliwa na Villa.