McCarthy apokezwa mikoba ya ukocha kambini mwa APOEL FC Nicosia ya Cyprus
Na MASHIRIKA
ALIYEKUWA kocha wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland, Mick McCarthy ameteuliwa kuwa mkufunzi wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Cyprus, APOEL Nicosia kwa mkataba unaotarajiwa kutamatika rasmi mnamo Mei 2022.
McCarthy, 61, amewahi pia kudhibiti mikoba ya vikosi vya Wolves na Ipswich. Aliagana rasmi na timu ya taifa ya Ireland mnamo Aprili 2020.
McCarthy alihudhuria mchuano wa APOEL dhidi ya Apollon mnamo Novemba 1, 2020 kabla ya kupokezwa rasmi mikoba ya kikosi hicho mnamo Novemba 2, 2020.
Msaidizi wake, Terry Connor, aliwahi kufanya naye kazi katika kikosi cha Wolves, Ipswich na timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland.
“Tunakaribisha kikosini wakufunzi wapya wa APOEL na kuwatakia kila la heri wanapojiandaa rasmi kwa majukumu yao. Lengo letu ni kuendelea kutwaa mataji ya haiba kubwa katika soka ya Cyprus na kupiga hatua zaidi katika kipute cha bara Ulaya,” ikasema sehemu ya taarifa ya APOEL.
Ingawa APOEL ndicho kikosi kinachojivunia ufanisi mkubwa zaidi katika historia ya soka ya Cyprus, kimeanza kampeni za msimu huu vibaya na kwa sasa wanashikilia nafasi ya 10 kwa alama tisa pekee kutokana na mechi nane zilizopita.
Rekodi ya mechi nne bila kusajili ushindi wowote ilikuwa kiini cha kocha raia wa Ugiriki, Marinos Ouzounidis ambaye ni kocha wa 12 wa APOEL tangu 2015.
Mechi ya kwanza ya McCarthy ni kibarua cha Ligi Kuu kitakachowakutanisha APOEL na Ethnikos Achna wanaokokota nanga mkiani mwa jedwali.
Stephen Kenny aliaminiwa kuwa mrithi wa McCarthy ambaye alidhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Ireland kwa awamu ya pili miezi sita iliyopita.