Mchezaji azimia uwanjani Oserian wakipiga Kayole Starlets
Na GEOFFREY ANENE
TIMU ya Oserian Ladies kutoka mjini Naivasha imetoka chini bao moja na kupapura wenyeji Kayole Starlet 4-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake ambayo mchezaji Sharon Juma kuzimia uwanjani Stima Club jijini Nairobi, Jumapili.
Kila timu ilishambulia ngome ya mwenzake mapema katika mchuano kabla ya Patricia Lesly kuweka Kayole kifua mbele dakika ya 16 baada ya kutokea msongamano kwenye lango la Oserian. Hellen Akinyi alipiga korna safi ambayo iling’ang’aniwa ndani ya kisanduku kabla ya Lesly kuielekeza wavuni.
Oserian, ambayo ilikuwa imekung’uta Kayole Starlet 4-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza Machi 9, iliamshwa kutoka usingizini na bao hilo. Baada ya kupoteza kona mbili zikifuatana, Oserian ilisawazisha 1-1 dakika ya 23 kupitia penalti ya nahodha Dorcas Shikobe.
Mchezaji huyu wa timu ya taifa alipata fursa hiyo Christine Ngoizi aliponawa mpira ndani ya kisanduku cha Kayole akiondosha hatari. Kipa Sharon Miloya aligusa mkwaju wa Shikobe kwa vidole, lakini ulikuwa mzito na kujaa wavuni.
Lesly alikuwa mwiba kwa Oserian, ambayo ilikuwa hatari kila wakati ilipokuwa ikienda mbele. Wageni Oserian walinufaika kuchukua uongozi 2-1 baada ya Kayole kujifunga bao ambalo lilipewa Sylvia Shilabukha aliyekuwa amevuta shuti hilo. Mchezaji wa Harambee Starlets Rebecca Akinyi alichangia pakubwa katika bao hili baada ya kusumbua pembeni kushoto kabla ya kuvuta krosi ndani ya kisanduku.
Kayole ilipata fursa ya kufanya mabao 2-2 dakika chache baadaye, lakini Ngoizi akapiga nje penalti iliyopatikana baada ya mchezaji wa Oserian kunawa mpira.
Sekunde chache baadaye, Oserian karibu ipate bao la tatu, lakini Miloya alikuwa macho kupangua shuti la Shilabukha. Miloya aliokoa shuti lingine hatari sekunde chache baadaye kutoka kwa Shikobe ambaye alikuwa amepata krosi murwa kutoka kwa Esther Kwamboka.
Oserian ilienda mapumzikoni mabao 3-1 juu baada ya Shikobe kuacha hoi safu ya ulinzi ya Kayole iliodhani ameotea.
Wageni Oserian walipoteza nafasi kadhaa nzuri hasa kutoka kwa Shikobe ambaye vichwa vyake havikulenga goli.
Juma aliumia goti, lakini akaamua kuendelea na mechi baada ya kupokea matibabu. Dakika chache baadaye, aliondosha mpira uliokuwa ukielekea wavuni baada ya Miloya kuchengwa. Shilabukha alipachika bao la nne kwa urahisi walinzi wa Kayole pamoja na kipa walipokosa kuwasiliana vyema.
Mechi ilisimamishwa kwa muda katika dakika za lala-salama baada ya Juma kuanguka uwanjani na kuzimia kabla ya kufanyiwa huduma ya kwanza. Hata hivyo, ilichezwa dakika chache na kipenga cha mwisho kikalia.
MATOKEO
JULAI 20
Kisumu All Starlets 1-0 Eldoret Falcons (Moi Stadium)
Wadadia 1-3 Thika Queens (Mumias Sports Complex)
Vihiga Queens 0-2 Kibera Girls Soccer Academy (Mumias Sports Complex)
Makolanders 4-1 Mathare United Women (Camp Toyoyo)
JULAI 21
Gaspo Women 3-0 Nyuki Starlets (ushindi wa bwerere baada ya Nyuki Starlets kutoka Kakamega kukosa kufika uwanjani Ruiru Grounds, Kiambu)
Vihiga Queens 3-3 Thika Queens (Mumias Sports Complex, Kakamega)
Kayole Starlet 1-4 Oserian Ladies (Stima Club, Nairobi)
Zetech Sparks 1-0 Spedag (Ruiru Grounds, Kiambu)