Mchezaji mkongwe zaidi kuwahi kufungia Uhispania astaafu soka
Na CHRIS ADUNGO
MVAMIZI Aritz Aduriz ambaye ni mwanasoka mkongwe zaidi kuwahi kufunga bao ndani ya jezi ya timu ya taifa ya Uhispania, amestaafu rasmi kwenye ulingo wa soka.
Huku kipute cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kikiwa kimesitishwa kwa muda kutokana na corona, Aduriz mwenye umri wa miaka 39, anatarajiwa kubadilishiwa paja zima.
Sogora huyo kwa sasa ni mshambuliaji wa klabu ya Athletic Bilbao inayoshiriki kivumbi cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).
Aduriz alitarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Bilbao ambacho kilipangiwa kuvaana na Real Sociedad kwenye fainali ya Copa del Rey mnamo Aprili 2020 kabla ya shughuli zote za soka kusitishwa kutokana na virusi vya homa kali ya corona.
“Nimekuwa nikisema kwamba mchezo wa soka utamwacha mtu kabla ya mtu kuuacha,” akaandika Aduriz kwenye mtandao wake wa Twitter.
“Jana, madaktari walinieleza niende kumwona daktari ambaye alitakiwa kunifanyia upasuaji wa paja. Nilipendekezewa kupata paja la plastiki ambalo kwa sasa nitasalia kuwa nalo kipindi changu cha maisha ya humu duniani. Mwili wangu unahisi kutosheka na soka,” akatanguliza.
“Siwezi sasa kuwasaidia wachezaji wenzangu jinsi ambavyo ningependa au kwa namna ambavyo wanastahili. Haya ndiyo maisha ya mwanasoka. Upo wakati wa kuangika daluga na kuuaga ulingo, ni kawaida,” akasema.
Aduriz ambaye pia amewahi kuchezea Valencia na Mallorca anajivunia kufungia Bilbao jumla ya mabao 141 kutokana na mechi 296 katika mapambano yote.
Aidha, anajivunia kuwajibishwa na timu ya taifa ya Uhispania mara 13 na akawa mchezaji wa umri mkubwa zaidi kufungia bao kikosi hicho mnamo 2016 akiwa na umri wa miaka 35 na siku 275.