Mchuano kati ya Nairobi Stima na Posta Rangers kuamua timu ya kuingia Ligi Kuu
Na GEOFFREY ANENE
BAADA ya msimu wa kawaida wa Ligi ya Supa kukamilika Jumapili, macho sasa yanaelekezwa kwa mechi ya kutafuta timu itakayojaza nafasi ya 18 kwenye Ligi Kuu ya msimu 2019-2020.
Mechi hiyo inayotarajiwa kusakatwa kabla ya Ligi Kuu kuanza mwezi Agosti, itakutanisha Nairobi Stima na Posta Rangers.
Stima ilimaliza Ligi ya Supa katika nafasi ya tatu baada ya kuzidiwa na nambari mbili Kisumu All Stars kwa tofauti ya ubora wa magoli nayo Rangers ilikamilisha Ligi Kuu katika nafasi ya 16.
Stima, ambayo ilitoa mfungaji bora Dennis Oalo, iliingia mechi yake mwisho dhidi ya Eldoret Youth na nafasi sawa na Kisumu All Stars na viongozi Wazito ya kunyakua tiketi mbili za moja kwa moja ikimaliza katika nafasi ya pili.
Hata hivyo, matumaini yake yalizimwa pale Wazito walitwaa taji kwa kucharaza St Joseph Youth 7-1 nao Kisumu wakapatia Thika United dozi sawa na hiyo.
Wanaumeme wa Stima waliridhika katika nafasi ya tatu kwa kulemea Eldoret 4-2. Tarehe za mechi kati ya Stima na Rangers bado hazijatangazwa pamoja na uwanja utakaotumika.
Waandalizi wa Ligi Kuu, kampuni ya KPL, pamoja na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) wanatarajiwa kutoa habari za mechi hizo wakati wowote.
Huenda Stima na Rangers wakavaana mwezi huu ama mapema mwezi ujao kwa sababu timu zinatarajiwa kuwa na mapumziko ya karibu wiki tatu kabla ya kuanza mipango ya msimu mpya.
Mshindi kati ya Stima na Rangers ataungana na Wazito na Kisumu All Stars waliochukua nafasi za Vihiga United na Mount Kenya United waliotemwa kutoka Ligi Kuu.
Timu zingine zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu 2019-2020 ni Gor Mahia, Bandari, Sofapaka, SoNy Sugar, Mathare United, Tusker, Kakamega Homeboyz, KCB, Ulinzi Stars na Kariobangi Sharks zilizofuatana katika nafasi 10 za kwanza msimu uliopita. AFC Leopards, Nzoia Sugar, Western Stima, Chemelil Sugar na Zoo pia zilikamilisha ligi katika nafasi salama.
Mara ya kwanza
Nairobi Stima haijawahi kushiriki Ligi Kuu. Itakuwa mara ya kwanza kabisa ikishinda Rangers, ambayo iliingia Ligi Kuu kwa mara ya kwanza mwaka 2010. Rangers ilitemwa mwaka 2012 kabla ya kurejea Ligi Kuu mwaka 2016.
Olalo alichangia mabao 12 ya Kisumu All Stars katika mechi za mkondo wa kwanza na idadi sawa akiwa mchezaji wa Nairobi Stima. Mabao yake yote (24) yalikuwa machache na mabao manne pekee ambayo Rangers ilipata msimu wote (28).
Atategemewa zaidi katika kampeni ya Nairobi Stima kuingia Ligi Kuu.
Msimu 2018-2019 ulishuhudia Thika United, Green Commandos ya Shule ya Upili ya Kakamega Boys na Kangemi Allstars zikipoteza nafasi zao kwenye Ligi ya Supa baada ya kuimaliza katika nafasi tatu za mwisho.