Michezo

McTominay kusalia Old Trafford hadi 2025

June 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO Scott McTominay wa Manchester United, ametia saini mkataba mpya katika maelewano ambayo kwa sasa yatamdumisha uwanjani Old Trafford hadi mwishoni mwa Juni 2025.

Kurefushwa kwa kandarasi ya McTominay mwenye umri wa miaka 23 ni zao la kuimarika kwa kiwango cha makali yake uwanjani Old Trafford tangu awajibishwe kwa mara ya kwanza na kocha wa zamani Jose Mourinho dhidi ya Arsenal mnamo Mei 2017.

Kwa kuwa yeye ni mzaliwa wa Lancaster, McTominay ni mchezaji wa timu ya taifa ya Scotland.

“Nimekua hadi kufikia hapa nilipo nikifahamu Man-United pekee maishani mwangu. Ni matumaini yangu kwamba mapenzi yangu kwa Man-United yatazidi kujidhihirisha yenyewe kila mara nitakapozidi kushuka uwanjani kuwawajibikia,” akatanguliza.

“Nitaendelea kuiwajibikia klabu hii kwa mapenzi ya dhati kila mara, niwe katika kikosi cha kwanza au la,” akasema.

Chipukizi huyo aliyeanza kupokezwa malezi ya soka akiwa katika akademia ya Man-United kwa sasa anajivunia kuchezeshwa na waajiri wake katika jumla ya michuano 75 ambapo amefunga mabao sita katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) likiwemo la pili katika ushindi wa 2-0 uliosajiliwa na Man-United dhidi ya Manchester City kwenye gozi la Machi 2020.

Kwa upande wake, kocha Ole ameshikilia kwamba McTominay atasalia kuwa mhimili muhimu kambini mwa Man-United kadri kikosi hicho kinavyopania kuanza kujinyakulia mataji ya haiba.

“Scott ni sehemu muhimu zaidi katika mipango yetu ya baadaye. Ni miongoni mwa chipukizi wanaojivunia utajiri mkubwa wa vipaji na amechangia kuinuka kwa ushindani mkali miongoni mwa wachezaji kambini,” akasema Solskjaer.