Meltah Kabiria waimumunya Kawangware United 4-0
Na JOHN ASHIHUNDU
Michuano ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Super 8 iliingia wiki ya 17, kwa mechi nae zilizochezewa katika viwanja mbalimbali, Kaunti ya Nairobi.
Ushindi wa Meltah Kabiria wa 4-0 dhidi ya Kawangware United katika mechi iliyochezewa Riruta Stadium, Jumapili umewapandisha hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Kufuatia matokeo hayo, Kabiria wanajivunia jumla ya pointi 29, mbili tu nyuma ya Githurai All Stars walio na 31 baada ya ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Makadara Junior League SA , huku Jericho All Stars wakiwa kileleni kwa pointi 33.
Baada ya kuanza mkondo wa pili kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Lebanon FC 1-0, Kawangware ambao ndio mabingwa wa taji la 2017 walitarajiwa kulipiza kisasi cha 4-1 walichopokea kutoka kwa Meltah lakini mipango yao haikufaulu walipojikuta wakibakia mkiani mwa jedwali.
“Tulijipanga vyema kwa vile ni mechi kubwa iliyowakutanisha majirani na juhudi zetu zimezaa matunda,” alisema kocha Paul Kamau wa Meltah.
Naibu kocha wa Kawangware, Laban Mwangi alikiri kwamba kuna presha kubwa kwa wachezaji wake ambao kwa sasa wanapigania kuhepa kuteremshwa ngazi.
“Tulianza vizuri, lakini wachezaji wakachanganyikiwa mechi ilipozidi kuendelea, tulitaka ushindi lakini bahati haikuwa yetu. Tuko katika nafasi mbaya na lazima tupigane vikali.”
Matokeo kwa ufupi yalikuwa: MASA 0-0 Jericho All Stars, Githurai All Stars 2-0 Makadara Junior League SA, Team Umeme 0-0 TUK, NYSA 1-0 Shauri Moyo Sportiff, Dagoretti Former Players FC 2-0 Mathare Flames, Kawangware United 0-4 Meltah Kabiria, Lebanon FC Rongai All Stars na Metro Sports 2-3 Huruma Kona