Messi atawazwa mfumaji hodari Uhispania
Na CHRIS ADUNGO
LIONEL Messi alijinyakulia taji la mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa mara saba mfululizo baada ya kuwafunga mabao mawili na kusaidia Barcelona kuwapepeta Alaves 5-0 katika mchuano wa mwisho wa kampeni za msimu huu mnamo Julai 19, 2020.
Mshambuliaji na nahodha huyo wa Barcelona alifunga msimu wa La Liga kwa mabao 25, manne zaidi kuliko Karim Benzema wa Real Madrid aliyekuwa mpinzani wake mkuu.
Hata hivyo, ushindi huo mnono wa Barcelona haukuwa wa manufaa sanaa kwa kikosi hicho cha kocha Quique Setien kwa kuwa Real Madrid walikuwa tayari wametawazwa mabingwa wa La Liga mnamo Julai 16 baada ya kuwachabanga Villarreal 2-1 uwanjani Alfredo Di Stefano.
Messi aliwafungulia Barcelona ukurasa wa mabao kunako dakika ya 34 kabla ya kupachika wavuni goli la tano katika dakika ya 75 baada ya Ansu Fati, Luis Suarez na Nelson Semedo kufunga mengine.
Riqui Puig, Messi na Arturo Vidal walishuhudia makombora yao langoni pa Alaves yakigonga mwamba wa goli.
Hii ni mara ya kwanza kwa mfungaji bora wa La Liga kupachika wavuni chini ya mabao 30 kwa msimu mmoja tangu Daniel Guiza wa Mallorca atikise nyavu za wapinzani mara 24 na kutwaa kiatu cha dhahabu miaka 12 iliyopita.
Barcelona kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Napoli ya Italia katika mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti 8, 2020 uwanjani Camp Nou. Mechi ya mkondo wa kwanza ulikamilika kwa sare ya 1-1 nchini Italia mnamo Februari 25, 2020.
MATOKEO YA LA LIGA (Julai 19, 2020):
Alaves 0-5 Barcelona
Leganes 2-2 Real Madrid
Valladolid 2-0 Real Betis
Villarreal 4-0 Eibar
Atletico 1-1 Real Sociedad
Espanyol 0-0 Celta Vigo
Granada 4-0 Athletic Bilbao
Levante 1-0 Getafe
Osasuna 2-2 Mallorca
Sevilla 1-0 Valencia