Michezo

Messi azamisha chombo cha Girona

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alifunga mabao mawili na kusaidia Barcelona kuwapepeta Girona FC 3-1 katika mchuano wa kujifua kwa minajili ya kampeni za msimu mpya.

Messi, 33, alirejelea mazoezi kambini mwa Barcelona wiki iliyopita baada ya uhamisho wake kutoka ugani Camp Nou hadi Manchester City ya Uingereza kutibuka.

Mabao yote mawili yalifungwa na Messi dhidi ya Girona waliowahi kumpa hifadhi mvamizi Michael Olunga wa Harambee Stars, yalielekezwa kimiani nje ya hatua ya 18.

Nahodha na fowadi huyo wa timu ya taifa ya Argentina alihusika pia katika bao la ufunguzi lililofungwa na Philippe Coutinho katika mechi hiyo iliyochezewa Francisco Trincao. Messi aliondolewa uwanjani katika dakika ya 60.

Barcelona wanatarajiwa kuanza kampeni zao za muhula mpya katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) dhidi ya Villarreal ya kocha Unai Emery mnamo Septemba 27, 2020 ugani Camp Nou.

Messi ambaye ni mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Barcelona, aliwawasilishia vinara wa Barcelona ombi la kutaka kubanduka ugani Camp Nou mnamo Agosti 2020 ila jaribio lake likatibuka.

Hii ni baada ya kukosekana kwa klabu iliyokuwa radhi kuweka mezani Sh89 bilioni ili kumsajili kwa mujibu wa kifungu kilichokuwa kwenye mkataba wake.

Messi alikuwa pia sehemu ya masogora waliotegemewa na kocha mpya Ronald Koeman katika mechi ya kirafiki iliyokutanisha Barcelona na Gimnastic de Tarragona. Barcelona waliibuka na ushindi wa 3-0 katika mechi hiyo baada ya kufungiwa na Ousmane Dembele, Antoine Griezmann na Philippe Coutinho.

Mnamo Septemba 16, Barcelona waliwajibisha jumla ya wanasoka 20 dhidi ya Girona ila fowadi Luis Suarez ambaye ni raia wa Uruguay na kiungo Arturo Vidal wa Chile wakasalia nje ya kikosi hicho.

Mapema Jumatano ya Septemba 16, Rais wa La Liga, Javier Tebas alisema anafurahishwa sana na maamuzi ya Messi kusalia ugani Camp Nou kuchezea Barcelona.