• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Barcelona wapepeta Ferencvaros 5-1 Messi na Fati wakiweka rekodi mpya UEFA

Barcelona wapepeta Ferencvaros 5-1 Messi na Fati wakiweka rekodi mpya UEFA

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi aliweka rekodi ya kufunga bao kwenye msimu wake wa 16 katika UEFA baada ya kusaidia Barcelona kupepeta Ferencvaros TC ya Hungary 5-1.

Mechi hiyo ilimpa chipukizi Pedro Gonzalez Lopez, 17, fursa ya kufungua rasmi akaunti yake ya magoli katika kikosi cha watu wazima kambini mwa Barcelona ambao kwa sasa wananolewa na kocha Ronald Koeman.

Messi alifuma penalti katika dakika ya 27 kabla ya miamba hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kufungiwa mabao mengine kupitia kwa Ansu Fati, Philippe Coutinho, Ousmane Dembele, Gonzalez na Gerard Pique aliyeonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 68.

Kuondolewa kwa Pique uwanjani kuliwapa Ferencvaros nafasi ya kufutiwa machozi na Ihor Kharatin katika dakika ya 70. Kadi nyekundu ambayo Pique alipokezwa ilikuwa yake ya pili baada ya meci 117 za UEFA na ilikuwa ya kwanza tangu Oktoba 2017 dhidi ya Olympiakos.

Barcelona waliendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa kwenye mechi 37 zilizopita za UEFA katika uwanja wao wa nyumbani wa Camp Nou. Mabingwa hao mara tano wa UEFA wamesajili ushindi mara 33 na kuambulia sare nne kwenye gozi hilo la bara Ulaya.

Tangu wapepete Grasshopper Club Zurich ya Uswisi kwenye UEFA kwa mara ya kwanza mnamo Septemba 1995, Ferencvaros hawajwahi kuibuka na ushindi mwingine kwenye kivumbi hicho kutokana na mechi sita zilizopita ambazo zimewashuhudia wakila sare mbili, kulazwa mara nne na kufungwa mabao 24.

Barcelona kwa sasa wamesajili ushindi mara 23 kutokana na mechi 25 zilizopita za ufunguzi wa kampeni za UEFA tangu walazimishiwe sare mbili na AC Milan mnamo 2011 na 2012.

Fati amefunga mabao manne kutokana na mechi tano katika mapambano yote yaliyopita msimu huu. Idadi hiyo ya mabao ndiyo kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kambini mwa Barcelona tangu 2020-21.

Chipukizi huyo mzawa wa Guinea-Bissau na raia wa Uhispania ndiye wa kwanza kuwahi kufunga mabao mawili ya UEFA kabla ya kutimu umri wa miaka 18.

Kwa upande wao, Barcelona ndicho kikosi cha kwanza cha bara Ulaya kuwahi kujivunia chipukizi wawili wasiozidi umri wa miaka 18 (Gonzalez na Fati) wakifunga mabao kwenye gozi moja la UEFA.

  • Tags

You can share this post!

Kipa Mendy ang’aa licha ya Chelsea kula sare ya...

Jinsi ya kuzuia saratani ya matiti