Mfumaji Diogo Jota atua Liverpool kwa Sh5.7 bilioni
Na MASHIRIKA
FOWADI Diogo Jota amejiunga na Liverpool kutoka Wolves kwa mkabata wa miaka mitano utakaorasimishwa leo (Jumamosi ya Septemba 19, 2020) kwa kima cha Sh5.7 bilioni.
Kusajiliwa kwa Jota, 23, kunadhihirisha ukubwa wa kiu ya kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp kuhifadhi ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu na kupiga hatua kubwa zaidi katika mashindano mengine ya Uingereza na bara Ulaya.
Fedha ambazo Liverpool huenda wakatoa kwa minajili ya huduma za Jota zinatarajiwa kuongezeka hadi Sh6.3 bilioni iwapo sogora huyo raia wa Ureno atawajibishwa mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha Liverpool na iwapo atachangia mafanikio makubwa ya Liverpool nchini Uingereza na barani Ulaya.
Wepesi wa Wolves kukubali fedha za uhamisho wa Jota kulipwa kwa awamu ulichangia pakubwa kufaulu kwa usajili wa mwanadimba huyo atakayetua ugani Anfield siku chache baada ya Liverpool kumsajili kiungo matata raia wa Uhispania, Thiago Alcantara kutoka Bayern Munich ya Ujerumani kwa Sh2.8 bilioni.
Jota anatazamiwa kufanyiwa vipimo vya afya ugani Melwood mnamo Septemba 19, 2020 kabla ya kutia saini mkataba atakapokezwa na Liverpool.
Jota aliondoka ugani Molineux kabla ya mchuano wa Carabao Cup uliowakutanisha Wolves na Stoke City mnamo Septemba 17 na alikuwa mchezaji wa akiba ambaye hakuwajibishwa kabisa katika gozi la EPL lililowashuhudia waajiri wake wakiwazaba Sheffield United 2-0 mnamo Septemba 13, 2020 ugani Bramall Lane.
Kuhamia kwa Jota ugani Anfield kulirahisishwa pia na hatua ya beki chipukizi wa Liverpool, Ki-Jana Hoever kukubali kuingia katika sajili rasmi ya Wolves kwa kima cha Sh1.4 bilioni.
Tineja huyo mwenye umri wa miaka 18 alichezeshwa na Liverpool mara nne pekee katika msimu wa 2019-20.
Alijiunga na Liverpool mnamo 2018 baada ya kuagana na Ajax ya Uholanzi na kutia saini mkataba wa kipindi kirefu ugani Anfield.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO