Miamba Tunisia walivyofunzwa kabumbu na limbukeni Namibia
Tunisia ilijipata ikiangukia pua mbele ya limbukeni Namibia baada ya kupokea kichapo cha 1-0 kwenye Kundi E ugani Amadou Gon Coulibaly mjini Korhogo.
Bao lililozamisha matumaini ya vigogo hao kutoka Afrika Kaskazini lilifungwa na Deon Hotto anayechezea klabu ya Orlando Pirates nchini Afrika Kusini. Hotto alifunga bao hilo kwa kichwa baada ya kuunganisha pasi ya Bethuel Muzeu.
Kichapo hicho kimewashusha mabingwa hao wa zamani hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo linaloongozwa na Mali ambao walianza kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Afrika Kusini wanaoshikilia nafasi ya mwisho.
Katika mechi hiyo, Namibia maarufu kama Brave Warriors walionekana kuzidiwa kwa kila idara, lakini Tunisia watajilauamu kwa kushindwa kufunga mabao hata walipofika kwenye kijsanduku cha hatari.
Kocha wao Jalel Kadri alifanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji na kuzidi kutawala mchezo huo hadi mwisho lakini bahati haikusimama.
Kadri alisema vijana wake walitengeneza nafasi nyingi ila walishindwa kuzitumia. “Tumeyakubalia matokeo haya kwa uchungu, lakini tumejifunza mengi. Wachezaji walionyesha juhudi zao lakini hatukuwa na bahati.”
Mabingwa hao wa zamani maarufu kama Carthage Eagles sasa watatakiwa kuupanda mlima kwenye mechi ijayo ili warejeshe matumaini ya Tunisia watashuka uwanjani Jumamosi kucheza na Mali kabla ya kumalizana na Afrika Kusini baadaye katika mechi ya mwisho ya kundi E.
Namibia pia walipoteza nafasi kadhaa, huku kipa Bechir Ben Said wa Tunisia akinyaka makombora kutoka kwa washambuliaji akiwemo nahodha Peter Shalulile anayechezea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Kipa wao Lloyd Kazapua alivuruga juhudi za washambuliaji wa Tunisia kwa kuokoa hatari kadhaa kutoka kwa washambuliaji wa Tunisia ambayo ni miongoni mwa timu zinazopigiwa upatu kutwaa ubingwa wa michuano hii.
Kabla ya ushindi huo, Namibia walikuwa hawajashinda mechi yoyote katika mashindano haya ya Afcon, baada ya kutoka sare mara mbili na kushindwa mara saba.
Kocha wao, Collins Benjamin ameweka historia kwa kuongoza nchi yake kupata ushindi wa kwanza katika fainali za Afcon, ushindi ambao ulishangiliwa kwa nderemo na vifijo nchini humo.
Ni ushindi ambao uliwashangaza mashabiki wengi kote duniani ikikumbukwa kwamba Tunisia inakamata nafasi ya 77 kwenye ubora wa viwango vya Fifa wakati Namibia wakiwa katika nafasi ya 115 katika orodha hiyo.
Tunisia walishinda ubingwa wa Afcon mnamo 2004 mashindano hayo yalipoandaliwa nchini humo, Kenya ikiwa miongoni mwa timu zilizoshiriki. Hii ni mara ya 16 kwa nchi hiyo kushiriki katika mashindano haya, ikitinga robo-fainali mara tatu na nusu-fainali mara nne, mbali na kumaliza katika nafasi ya nne mnamo 2019.