Michuano ya Chapa Dimba wikendi
Na JOHN KIMWERE
Mashindano ya Chapa Dimba na Safaricom Season Three wikendi hii yatashuhudia fainali za Mkoa wa Nairobi, ambazo zimepangwa kuchezewa katika uwanja wa Shule ya Upili ya Jamhuri High.
Mabingwa watetezi kitengo cha wavulana, South B Allstars itakosekana baada ya kushindwa kunasa tiketi ya kushiriki fainali za msimu huu.
Upande wa wasichana, Acakoro Ladies itakuwa nga’ang’ari kutetea ubingwa huo ili kuwakilisha Mkoa wa Nairobi kwa mara ya pili katika fainali za kitaifa. Mechi za nusu fainali zitachezwa Jumamosi nazo fainali zitaandaliwa Jumapili.
Kwenye nusu fainali ya wasichana St Annes Eaglets kutoka Makadara italimana na Acakoro Ladies ya Kasarani, nayo Kibagare Girls itamenyana na Beijing Raiders ya Starehe.
Kwa wavulana Hakati Sportiff ya Makadara itashuka dimbani kuchuana na BVrookshine Academy ya Kasarani. Nao chipukizi wa KSG Ogopa kutoka Westlands watakutanishwa na Dagoretti Mixed Boys.
”Muhula Mkoa wa Nairobi ulishirikisha zaidi ya timu 100 zilizoshiriki mashindano hayo kupigania tiketi za kushiriki fainali za Kitaifa,” alisema mshirikishi wa kipute hicho, James Omondi pia alitoa mwito kwa wachezaji wa timu zote wazingatie nidhani zaidi.
Mabingwa wa taji hilo, kitengo cha wavulana na wasichana watajikatia tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa ambazo zimepangwa kuandaliwa mjini Mombasa Mwezi Juni mwaka huu.
Kando na hayo, timu hizo mbili kila moja itapokea kitaita cha Sh200,000. Nazo timu zitakaomaliza katika nafasi mbili kila moja itapoongezwa kwa Sh100,000.
Washindi wa eneo hilo watajiunga na wenzao kutoka maeneo mengine kufuzu kwa fainali za kitaifa. Wavulana watajiunga na wenzao wa Berlin FC ya Garissa (Mkoa wa Kaskazini Mashariki, Ulinzi Youth ya Mkoa wa Kati , Tumaini school (Mkoa wa Mashariki)na Yanga FC kutoka Malindi Mkoa wa Mombasa.
Wasichana watajiunga na Falling Waters Mkoa wa Kati, Isiolo Starlets (Mkoa wa Mashariki) na Kwale Ladies malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.