Michezo

Migne aahidi kuisuka upya Harambee Stars

July 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN ASHIHUNDU

MARA tu baada ya kichapo cha 3-0 kutoka kwa Senegal jijini Cairo, kocha Sebastien Migne wa Harambee Stars ametangaza mipango ya kuisuka upya timu hiyo ya taifa kwa ajili ya mashindano ya usoni.

Matokeo hayo ya Jumatatu usiku yalididimiza nafasi ya kikosi cha Migne kusonga mbele katika michuano ya AFCON inayoendelea nchini Misri, ingawa mashabiki wengi walikuwa wakisubiri kwa hamu matokeo ya mechi za mwisho za makundi zilizochezwa Jumanne usiku.

Kulingana na Migne, kikosi cha mechi zijazo kitaundwa na wachezaji wengi wa umri mdogo, huku akifafanua kwamba mastaa wengi wakongwe wataondolewa wakati ataanza kujenga timu mpya ya kushiriki katika michuano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia na lile la AFCON.

“Wakati tunasubiri matokeo ya mechi zilizosalia, nimetambua vijana kadhaa ambao nitawajumuisha katika kikosi cha usoni kwa ajili ya mechi za kimataifa,” Migne alinukuliwa kupitia kwa mtandao wa CAF.

Harambee Stars ilimaliza mechi za Kundi C baada ya kujikusanyia pointi tatu kufikia Jumanne, japo ilikuwa ikitegemea Ghana, Mali na Cameroon zishinde mechi zao ili ifuzu kwa hatua ya 16 Bora.

DR Congo na Afrika Kusini zilimaliza kwa pointi tatu kila moja, wakati Guinea ikijivunia pointi nne.

Timu zilizokuwa zimefuzu moja kwa moja hadi hatua ya 16 Bora kabla ya mechi za Jumanne usiku ni wenyeji Misri, Madagascar, Algeria na Morocco.