Migne afichua siri ya kuzima Algeria na Senegal Afcon
Na CHRIS ADUNGO
KIKOSI cha Harambee Stars kinatarajiwa kuondoka jijini Paris, Ufaransa mwishoni mwa wiki hii na kuelekea Madrid, Uhispania kupimana nguvu na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Stars watashuka dimbani kwa minajili ya mechi hiyo baada ya kuwachabanga Madagascar 1-0 katika mechi nyingine ya kirafiki iliyowakutanisha jijini Paris wikendi iliyopita.
Kiungo na nahodha wa Stars Victor Wanyama ambaye kwa sasa huchezea Tottenham Hotspur ya Uingereza ndiye aliyekuwa mfungaji wa bao hilo la pekee lililotokana na mkwaju wa penalti.
Mchuano dhidi ya DR Congo utakuwa wa mwisho kwa Stars kupima kiwango cha maandalizi yao kabla ya kutua jijini Cairo, Misri kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Juni 19.
Ina maana kwamba Stars watakuwa na siku tano pekee za kuzoea joto jingi la Misri, tofauti na baridi kali ambayo kwa sasa inashuhudiwa nchini Ufaransa wanakopiga kambi ya mazoezi.
Stars wamepangwa katika Kundi C pamoja na Senegal, Algeria na majirani zao katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania.
Chini ya Migne, Stars watafungua kampeni za makundi dhidi ya Algeria mnamo Juni 23 kabla ya kuchuana na Tanzania siku nne baadaye. Watamenyana na Senegal mnamo Julai 1. Mechi zote za Stars katika hatua hii ya makundi zitatandazwa ugani June 30 jijini Cairo.
Baada ya kufichua kikosi cha wachezaji 23 atakaowategemea nchini Misri, mikakati ya Migne katika fainali za AFCON mwaka huu pia zimebainika.
Migne ambaye ni mzaliwa wa Ufaransa, aliwadumisha kambini makipa watatu, mabeki wanane, viungo tisa na mafowadi watatu kwa minajili ya fainali hizo ambazo huandaliwa kila baada ya miaka miwili.
Kocha huyo aliyewahi kuwa msaidizi wa veterani Claude Leroy nchini Congo, aliwatema jumla ya wachezaji wanne.
Mbali na Brian Mandela na Christopher Mbamba waliopata majeraha wakiwa mazoezini, Migne pia aliwatupa nje kiungo Anthony Akumu na Clifton Miheso ambao kwa sasa wanapiga soka ya kulipwa nchini Zambia na Ureno mtawalia.
“Ukiangalia kikosi ambacho kimeteuliwa na Migne, utaona kwamba atapania kuwawajibisha wachezaji walio na mazoea ya kubana sana. Migne atalenga sana kuzuia badala ya kuvamia. Utagundua kwamba mikakati yake ni kusuka njama ya kuzima makali ya Senegal na Algeria ambao hushambulia zaidi,” akasema kocha wa zamani wa Stars, James Nandwa.
“Masoud Juma, John Avure, Ovella Ochieng, Paul Were, Eric Johanna na Ayub Timbe ni wachezaji chipukizi ambao wana nguvu ya kuwania mpira kutoka kwa wapinzani, kupiga chenga na kushambulia kwa kushtukiza.
Kasi yao itawasaidia kumpokeza Michael Olunga pasi nyingi kwa urahisi,” akaongeza.
Katika safu ya kati, tajriba ya Wanyama na Francis Kahata itahitajiwa sana ili kusuka pasi zitakazochangia krosi za kumfikia Olunga katika idara ya mbele.
Ni matumaini ya Migne kwamba mabeki Musa Mohamed, Joash Onyango, Aboud Omar na Philemon Otieno watashirikiana vilivyo na Dennis Odhiambo na Johanna ‘Tosh’ Omollo kuyeyusha presha ya wapinzani hasa watakapochuana na Senegal wanaojivunia wavamizi stadi kama vile Sadio Mane, Ismailia Sarr na Keita Balde.
Mbinu hii ya Migne iliwahi kufaulu Stars walipopepetana na Ghana katika mojawapo ya mechi za kufuzu kwa fainali za AFCON jijini Nairobi. Stars walivuna ushindi wa 1-0 katika mchuano huo wa Septemba 2018.
Kikosi cha stars
Makipa: Patrick Matasi, John Oyemba, Faruk Shikalo
Mabeki: Philemon Otieno, Abud, Bernard Ochieng, Musa Mohammed, Joash Onyango, Joseph Okumu, David Owino, Eric Ouma.
Viungo: Victor Wanyama, Dennis Odhiambo, Erick Johanna, Ayub Timbe, Francis Kahata, Ismael Gonzalez, Ovella Ochieng, Paul Were, Johanna Omollo.
Wavamizi: Masoud Juma, Michael Olunga, John Avire.