Michezo

Migne ataja kikosi cha kutafutia Kenya tiketi ya CHAN 2020

July 26th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Sebastien Migne ametaja kikosi chake cha mwisho kitakachovaana na Taifa Stars ya Tanzania jijini Dar es Salaam hapo Julai 28 katika mechi ya mkondo wa kwanza ya kufuzu kushiriki soka ya Afrika ya wachezaji wanaosakata katika mataifa yao (CHAN) mwaka 2020.

Beki Johnstone Omurwa, 20, ambaye alijumuishwa katika kikosi cha kufanya mazoezi katkati mwa juma, pamoja na kiungo chipukizi Musa Masika, 18, wamepata namba katika kikosi cha wachezaji 22.

Musa Masika ni nduguye mdogo wa winga matata wa Beijing Renhe, Ayub Timbe.

Beki Dennis Odhiambo, 34, ambaye alikuwa mmoja wa wachezaji wenye umri wa juu kabisa katika Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri mwaka 2019, ametwikwa majukumu ya nahodha.

Migne na vijana wake wataondoka jijini Nairobi leo alasiri kuelekea Dar es Salaam kwa mechi hiyo ya raundi ya kwanza.

Kocha mpya wa timu ya Tanzania, Etienne Ndayiragije bado hajataja kikosi chake cha mechi hii ya raundi ya pili. Mechi ya marudiano ni jijini Nairobi mnamo Agosti 4.

Mshindi baada ya mikondo yote miwili atakabiliana na Sudan kati ya Septemba 20-22 na Oktoba 18-20 kujikatia tiketi ya kushiriki makala ya sita ya soka ya CHAN nchini Cameroon mwaka 2020.

Kikosi cha Kenya

Makipa: James Saruni (Ulinzi Stars), John Oyemba (Kariobangi Sharks);

Mabeki: Johnstone Omurwa (Mathare United), David Owino (Mathare United), Benard Ochieng (Wazito), Mike Kibwage (KCB), Joash Onyango (Gor Mahia);

Viungo: Duke Abuya (Kariobangi Sharks), Whyvone Isuza (AFC Leopards), Dennis Odhiambo (Sofapaka/nahodha), Kenneth Muguna (Gor Mahia), Ibrahim Shambi (Ulinzi Stars), Musa Masika (Wazito), Teddy Osok (Wazito), Abdalla Hassan (Bandari), Samuel Onyango (Gor Mahia), Clifton Miheso (Kenya Police), Patillah Omoto (Kariobangi Sharks);

Washambuliaji: Sydney Lokale (Kariobangi Sharks), Enosh Ochieng (Ulinzi Stars), Piston Mutamba (Wazito), Nicholas Kipkirui (Gor Mahia)