• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:19 PM
Miheso mwingi wa imani Stars itapiga TZ

Miheso mwingi wa imani Stars itapiga TZ

Na CECIL ODONGO

KIUNGO wa Harambee Stars Clifton Miheso ameeleza imani yake kwamba timu hiyo itashinda Tanzania kwenye mkondo wa pili wa mechi ya CHAN.

Stars ililazimisha sare tasa dhidi ya Taifa Stars ya Tanzania timu hizo zilipokutana kwenye mkondo wa kwanza jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita.

Matokeo hayo ni ishara kwamba timu yoyote kati ya Kenya na Tanzania ina uwezo wa kufuzu raundi ya pili kwenye kipute hicho kinachowashirikisha wachezaji wa ligi za nyumbani pekee.

Ingawa hivyo, Miheso ambaye anasakatia Police FC amesema ana wingu la matumaini kikosi cha timu ya taifa kitaibuka kidedea kwa kuwa kitatiwa shime na halaiki ya mashabiki wa soka watakaojitokeza uwanja wa MISC Kasarani Jumapili hii.

“Tutakuwa nyumbani na lazima tujitahidi ili kupata matokeo ya kuridhisha. Tuna imani mambo yatakuwa shwari hasa tukipata motisha kutoka kwa mashabiki. Asilimia kubwa ya kazi ilifanywa katika mkondo wa kwanza na kilichosalia ni kupiga msumari moto kwenye kidonda cha wapinzani kisha tusonge mbele,” akasema Miheso.

Alisema wamekuwa wakifanya mazoezi kwa njia inayofaa.

“Tumekuwa tukifanya mazoezi kabambe na tumejiandaa vilivyo kwa mtanange huo. Nafahamu kwa kuwa sisi ni timu ya nyumbani, tutakuwa na presha ya kupata ushindi japo nina imani hatutakosa ushindi. Hata hivyo, nakiri itakuwa mechi ngumu na timu itakayokosa kutumia nafasi zake vizuri itajilaumu yenyewe,” akaongeza Miheso.

Harambee Stars inayonolewa na Mfaransa Sebastien Migne italenga kuendeleza ubabe dhidi ya Tanzania hasa baada ya kocha mpya wa Taifa Stars Etienne Ndayiragije kuahidi kuwaonyesha kivumbi kwenye mkondo wa pili.

You can share this post!

Tangatanga wakunja mikia

SIONDOKI SPURS: Wanyama akariri haiachi klabu yake licha ya...

adminleo