Michezo

Militao kukosa mechi ya kufa kupona kati ya Real Madrid na Inter Milan kwenye UEFA

November 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

BEKI Eder Militao hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Real Madrid dhidi ya Inter Milan kwenye mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 3, 2020 baada ya kupatikana na ugonjwa wa Covid-19.

Nyota huyo raia wa Brazil mwenye umri wa miaka 22 kwa sasa atahitajika kujitenga kwa siku 14 zijazo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Real, Real ndiye wa pekee aliyepatikana na virusi vya corona kambini mwao baada ya wachezaji, maafisa wa benchi ya kiufundi na waajiriwa wengine wa kikosi hicho kufanyiwa vipimo vya corona.

Real ambao kwa sasa wanakokota nanga mkiani mwa Kundi B kwenye soka ya UEFA watakuwa wenyeji wa Inter kutoka Italia katika mechi ya tatu jijini Madrid, Uhispania.

Militao amewajibishwa na Real mara tatu hadi kufikia sasa msimu huu na aliridhisha sana katika mechi iliyoshuhudia Shakhtar Donetsk ikiwapokeza kichapo cha 3-2 mnamo Oktoba 21, 2020 jijini Madrid.

Real wamejizolea alama moja pekee kutokana na mechi mbili za kwanza za Kundi B kwenye kivumbi cha UEFA msimu huu baada ya kupoteza 3-2 dhidi ya Shakhtar na kuambulia sare ya 2-2 dhidi ya Borussia Monchengladbach ya Ujerumani mnamo Oktoba 27, 2020.