Michezo

Mipango ya Kuwinda United kwa msimu ujao

June 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kuwinda United inakiri kuwa licha ya kujikuta njia panda msimu huu kwenye mechi za Kundi A Ligi ya Kaunti ya FKF, Tawi la Nairobi Magharibi sasa inajipanga kutifua vumbi kali muhula ujao.

Viongozi wake wanaamini kuwa endapo watapa udhamini bila shaka watatesa wapinzani wengine kinyume na matarajio ya wengi na kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki michuano ya ligi za hadhi ya juu nchini miaka ijayo.

Wanasoka hao wanajivunia kushiriki mechi za Ligi ya Kaunti pia Ligi ya Mkoa ndani ya miaka minanne iliyopita ambapo wamekuwa wakipanda ngazi na kushuka.

Meneja wake, George Mungai anasema, ”Msimu huu tungekuwa moto wa kuotea mbali kwenye kampeni za Ligi ya Kaunti lakini mkasa wa moto ulioteketeza mtaa wa Kuwinda mwaka uliyopita ulivuruga mpango wetu.”

Ofisa huyo amedokeza kuwa kisa hicho kilifanya baadhi ya wachezaji wao kujipata bila makao na kuhamia kwingine pia wakisaka matunda mema. Katika mpango mzima anasema ukosefu wa udhamini pia umechangia kikosi hicho kutopiga hatua michezoni.

”Kusema kweli Kuwinda United ina wanasoka wazuri waliotunukiwa talanta ya kushiriki soka ya kimataifa lakini hatuna mfadhili jambo ambalo hufanya baadhi yao kuhamia kwingine kusaka posho,” alisema huku akitoa mwito kwa wahisani wajitokeza kusaidia timu za mashinani kupapalia vipaji vya wachezaji chipukizi.

Kuwinda United ambayo hutiwa makali na kocha, Samuel Kioko huchezea mechi zake katika uwanja wa Utume, Karen.

Kocha huyo anatoa shukrani za dhati kwa mfanyi biashara, Njoroge Mburu ambaye anasema amekuwa mstari wa mbele kuwashika mkono hasa kugharamia usafiri wao nyakati zote wanakosafiri kushiriki mechi za ugenini.

Licha ya kukutanishwa na changamoto kibao Kuwinda United inajivunia kukuza wachezaji kadhaa waliobahatika kusajiliwa na klabu tofauti kuzipigia kwenye ligi tofauti hapa nchini. Klabu hiyo imenoa makucha ya Paul Karuri ambaye husakatia FC Talanta ya Supa Ligi ya Taifa (NSL).

Kabla ya kutwaliwa na FC Talanta mchezaji huyo aliwahi kuzichezea timu tofauti ikiwemo KCB, Bidco United na Wazito FC.

Kuwinda United inajumuisha wanasoka kama: Daniel Mutuku, James Njoroge, Kelvin Ouma, Erick Kakunzu, Ibrahim Jaldesa, Samuel Ochieng, Edrick Kanara, Martin Kaptinga, Antony Awimbo, Papa Njoroge, John Kimani na Martin Kariuki. Pia wapo Collins Idea, Julius Karugu, Mathew Mungai, John Baraza, Alex Muyonga, Evans Mwangi na John Muriuki. Maofisa wake pia wapo Simon Ngige na Francis Chalo kati ya wengine.

Kocha huyo analitaka Shirikisho la Soka ya Kenya (FKF) Tawi la Nairobi Magharibi kutathimini kazi ya waamuzi wa mechi za ligi zote chini ya tawi hilo.

Anawaponda waamuzi wengine wenye kasumba ya kupendelea timu zingine na kukosa kutoa uamuzi inavyostahili dhidi ya wapinzani wao. Anasema hatua hiyo hufanya kiwango cha mchezo wa soka nchini kuendelea kudidimia badala ya kupiga hatua.