Michezo

Misri kuandaa kipute cha AFCON 2019

January 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE na CHRIS ADUNGO

MIAMBA wa soka barani Afrika, Misri wametangazwa kuwa wenyeji wa Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019.

Washindi hawa wa AFCON mara saba (1957, 1959, 1986, 1998, 2006, 2008 na 2010) walikuwa wakiwania uenyeji wa makala hayo ya 32 dhidi ya mabingwa wa mwaka 1996 Afrika Kusini baada ya Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) kupokonya mabingwa mara tano na watetezi Cameroon haki za kuyaandaa kwa kuchelewa kuweka vifaa vinavyotatikana na pia kwa salabu za kiusalama.

Misri imechaguliwa kuwa mwenyeji katika kikao cha maafisa wakuu wa CAF jijini Dakar, Senegal mnamo Jumanne.

Mashindano haya yatakayoshuhudia mataifa shiriki yakiongezwa kutoka 16 hadi 24, yatafanyika kutoka Juni 15 hadi Julai 13, 2019.

Kenya ni moja ya mataifa 14 yaliyofuzu kufikia sasa. Mataifa mengine yaliyojikatia tiketi kuwa Misri ni Wamisri wenyewe pamoja na Uganda, Tunisia, Mauritania, Ivory Coast, Guinea, Ghana, Nigeria, Algeria, Mali, Morocco, Senegal na Madagascar.

Mauritania na Madagascar zimefuzu kwa mara ya kwanza katika historia yao nayo Kenya inarejea baada ya kukosa makala saba yaliyopita.

Washiriki 10 waliosalia watafahamika wakati wa mechi za mwisho za mchujo mwezi Machi. Dimba la AFCON linarejea Misri baada ya miaka 13.

Ivory Coast, ambao walikuwa wawe wenyeji wa fainali hizo mnamo 2021, tayari wamewasilisha malalamiko yao kwa Jopo Maalum la CAF la kutatua mizozo ya spoti (CAS).

Mnamo Jumatatu, Shirikisho la Soka la Guinea lilitangaza kwamba lipo radhi kuhamisha uenyeji wao wa kipute cha AFCON hadi 2025 badala ya 2023.

Kenya watakuwa wakishiriki fainali za AFCON 2019 kwa mara ya kwanza baada ya miaka 14.

Kufuzu kwa Kenya kulitokana na maamuzi ya CAF kuitupa nje Sierra Leone kwa sababu za kiutawala na hivyo kuliacha Kundi F likiwa na timu tatu pekee.

Sierra Leone ilikuwa imecheza mechi mbili katika kampeni yao na kwa sababu haikuwa imekamilisha nusu ya mechi zote za kufuzu, CAF iliamua kufutilia mbali matokeo yote ya awali yaliyohusisha timu hiyo kulingana na kanuni za kufuzu.

Stars ilishiriki mashindano ya AFCON kwa mara ya mwisho mnamo 2004 chini ya kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee baada ya kupangiwa katika B pamoja na Senegal, Burkina Faso na Mali.

Kikosi cha Mulee wakati huo kiliungwa na makipa Francis Onyiso, Willis Ochieng na Duncan Ochieng. Walinzi walikuwa Andrew Oyombe, Musa Otieno, Philip Opiyo, Moses Gikenyi, George Waweru, Adam Shaban na Issa Kassim. Safu ya kati ilijivunia Robert Mambo, Walter Odede, Titus Mulama, John Muiruri, Anthony Mathenge na Emmanuel Ake huku mashambulizi yakiongozwa na masogora matata Mike Okoth, Maurice Sunguti, John Baraza, James Omondi na Dennis ‘The Men- ace’ Oliech ambaye kwa sasa anavalia jezi za Gor Mahia.