• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
Mitambo yamfungia Mkenya nje ya mbio za Birmingham

Mitambo yamfungia Mkenya nje ya mbio za Birmingham

Na GEOFFREY ANENE

HITILAFU ya kimitambo katika Balozi ya Uingereza nchini Marekani imefungia Mkenya Emmanuel Korir nje ya Riadha za Dunia zinazoendelea mjini Birmingham, Uingereza.

Korir, ambaye ni mkazi wa Marekani, alikuwa katika orodha ya Wakenya saba waliochaguliwa kushiriki mashindano hayo yaliyovutia mataifa 144. Alikuwa mwakilishi wa pekee wa Kenya katika mbio za mita 800.

Ziara yake nchini Uingereza haikufanyika baada ya kukosa stakabadhi za usafiri kutokana na hitilafu katika mitambo ya mawasiliano.

“Tungependa kuwashauri kwamba kwa wakati huu afisi zetu jijini New York zinakumbwa na matatizo ya kimitambo na simu zetu hazifanyi kazi,” balozi hiyo ya Uingereza ilitangaza Ijumaa.

Korir ni mmoja wa wakimbiaji ambao Kenya ilikuwa na matumaini makubwa itapata medali kutoka kwake.

Ni mara ya kwanza kabisa mkimbiaji mwanamume kutoka Kenya hajashiriki katika mbio za mita 800 tangu Riadha za Dunia za Ukumbini zianzishwe mwaka 1985.

Wawakilishi wengine wa Kenya mwaka 2018 ni Bethwell Birgen, David Kiplangat (mita 3000), Beatrice Chepkoech (mita 1500) na Winny Chebet (mita 800 na mita 1500), Vincent Kibet (mita 1500) na Hellen Obiri. Bingwa mbio za mita 3000 mwaka 2012, Obiri, hakuwa na lake katika siku ya kwanza ya mashindano hapo Machi 1 alipomaliza kitengo hiki katika nafasi ya nne.

You can share this post!

Walishwa kadi nyekundu kwa kuvunja sheria mbio za Birmingham

Pipeline na Prisons wazuiwa kufanyia mazoezi Kasarani

adminleo