Mkenya Duke Abuya asaidia Nkana kunyoa Kitwe United bila maji Ligi Kuu Zambia
Na GEOFFREY ANENE
KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya, Duke Abuya alimega pasi iliyozalisha bao, huku wenyeji Nkana wakizamisha Kitwe United 2-0 kwenye Ligi Kuu ya Zambia, Jumatano.
Mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Kariobangi Sharks alisaidia Nkana kupata bao la kwanza alipopasia Idriss Mbombo mpira ambao nahodha huyo alikamilisha kwa ustadi dakika ya 26.
Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mbombo aliimarisha uongozi wa Nkana dakika 13 baadaye baada ya kuiba pasi ya nyuma iliyopigiwa kipa.
Beki Mkenya Harun Shakava pia alijumuishwa katika kikosi cha wachezaji 11 wa kwanza wa Nkana ambayo imepaa nafasi mbili hadi nambari 12. Imezoa alama 11 baada ya kusakata mechi nane.
Mshambuliaji Mkenya Timothy Otieno pia alikuwa uwanjani Jumatano kusakatia NAPSA Stars kwenye ligi hiyo katika mchuano dhidi ya wenyeji Power Dynamos uliotamatika 2-2.
NAPSA Stars, ambao pia wameajiri kipa Mkenya Shaaban Odhoji, walitupa uongozi mara mbili katika sare hiyo. Odhoji alilishwa kadi ya njano kwa kupoteza muda kabla ya Benson Chali kusawazisha na kiki ya mwisho ya mechi katika dakika ya nne ya nyongeza.
NAPSA inapatikana katika mduara hatari wa kutemwa katika nafasi ya 16 kwenye ligi hiyo ya timu 18 kwa alama saba kutokana na michuano saba.
Ijumaa ya Desemba 18 itakuwa zamu ya Wakenya Ian Otieno (kipa), David Owino (neki) na washambuliaji Jesse Were na John Makwata kuwakilisha timu yao ya Zesco United dhidi ya Green Eagles. Zesco inashikilia nafasi ya pili nyuma kwa alama 18 kutokana na michuano 10. Buildcon iko juu kwa idadi sawa ya alama na mechi, lakini inajivunia tofauti ya ubora wa magoli.