Michezo

Mkimbiaji kupoteza Sh5.8 milioni na medali baada ya kupigwa marufuku kwa kutumia pufya

Na GEOFFREY ANENE November 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MTIMKAJI Emmaculate Anyango anaenda kupoteza zawadi za thamani isiyopungua Sh5,895,000 kutokana na madhambi ya kutumia dawa za kusisimua misuli ambazo zimefanya ampigwe marufuku miaka sita.

Mshindi wa nishani ya fedha mbio za mita 3,000 kwenye Riadha za Afrika za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka 2019 Anyango, 24, amepokea marufuku hiyo kutoka kwa Kitengo cha Maadili cha Shirikisho la Riadha Duniani (AIU) baada ya kupatikana na hatia ya kutumia dawa zilizopigwa marufuku za aina ya EPO pamoja na Testosterone.

Marufuku inaanza kutumika tangu Septemba 26, 2024

“Anyango anapoteza matokeo yote aliyopata kutoka Februari 3, 2024 hadi alipopatikana na hatia,” AIU ilitangaza kupitia mitandao yake ya kijamii.

Katika kipindi amepoteza matokeo, Anyango alishinda mbio za nyika za Sirikwa Classic mnamo Februari 3 uwanjani Lobo Village mjini Eldoret, akawa nambari mbili mbio za nyika za Idara ya Magereza katika Chuo cha Mafunzo cha Magereza (PSTC) mjini Ruiru, Kiambu mnamo Machi 2, akakamata nafasi ya nne Mbio za Nyika za Dunia mjini Belgrade, Serbia mnamo Machi 30, na akawa nambari mbili B.A.A. 5K mjini Boston, Amerika (Aprili 13).

Pia, Anyango alikamata nambari mbili Tata World 10K mjini Bengaluru, India (Aprili 28), nambari sita mbio za mita 10,000 kwenye riadha za Diamond League mjini Eugene, Amerika (Mei 25), nafasi ya nne mbio za Atlanta Journal-Constitution Peachtree Road Race nchini Amerika (Julai 4) halafu akamaliza Boilermaker 15K Road Race nambari mbili nchini Amerika (Julai 14).

Mshindi wa Sirikwa Classic alivuna Sh1.2 milioni (Dola za Amerika 10,000), Sh1.2m (Dola za Amerika 10,000) kutoka Belgrade, Sh518,000 (Dola za Amerika 4,000) kutoka B.A.A. 5K Boston, Tata World 10K Bengaluru akatia mfukoni Sh2.2m (Dola za Amerika 17,000), Sh259,000 (Dola za Amerika 2,000) kutoka Atlanta Journal-Constitution Peachtree Road Race, na Sh518,000 (Dola za Amerika 4,000) kutoka Boilermaker 15K Road Race.

Anyango alipimwa mkojo Februari 3, Machi 13 na Juni 2, na mkojo na damu mnamo Juni 16 ambazo baada ya kufanyiwa uchunguzi katika maabara ya Shirika la Kukabiliana na Matumizi ya Pufya (WADA) mjini Lausanne, Uswisi, alipatikana kutumia dawa hizo haramu.

“Kupoteza matokeo yote kutoka Februari 3, 2024 inamaanisha kuwa atapoteza medali zote, mataji yote, tuzo zote, pointi zote, zawadi, zawadi za kifedha na ada ya kujitokeza kushiriki mashindano,” AIU ilieleza ikitangaza marufuku dhidi ya Anyango.

Anyango alibahatika kupoteza muda wa pili bora duniani katika mbio za 10 barabarani mjini Valencia, Uhispania mwezi Januari 2024. Alikamilisha 10km mjini Valencia kwa dakika 28:57, nyuma ya Mkenya mwenzake Agnes Ngetich aliyeweka rekodi ya dunia 28:46.