Michezo

Mkufunzi wa Guinea ya Ikweta sasa ajiuzulu

October 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Angel Lopez wa Guinea ya Ikweta ameagana rasmi na kikosi hicho mwaka mmoja pekee tangu apokezwe mikoba ya timu ya taifa ya soka ya nchi hiyo.

Kulingana naye, kiini cha kujiuzulu kwake ni kutafuta changamoto mpya kwingineko.

Hatua hiyo inajiri siku chache baada ya timu hiyo kuwapepeta Sudan Kusini 2-1 katika mojawapo ya mechi za mchujo wa kufuzu kwa fainali za Kombe Dunia za 2022 nchini Qatar.

Ushindi huo uliwakatia tiketi ya kuchuana na Tanzania ugenini kabla ya kuwaalika Tunisia mnamo Novemba katika michuano mingine miwili zaidi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zitakazoandaliwa nchini Cameroon mnamo 2021.

Hadi alipojiuzulu, Lopez ambaye ni mzawa wa Uhispania, alikuwa amewaongoza Equatorial Guinea kusimamia mechi tisa.

Katika mojawapo ya mechi hizo, waliwapepeta Sudan 4-1 mnamo Machi 2019 kabla ya kusajili ushindi mara mbili zaidi, kutoka sare mara tatu na kupoteza jumla ya mechi tatu.

Lopez amewahi pia kudhibiti mikoba ya vikosi kadhaa nchini China, Romania na United Arab Emirates (UAE).

Alipoaminiwa kukiongoza chombo cha Guinea ya Ikweta jijini Malabo, alikuwa mkufunzi wa Recreativo Huelva inayoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili nchini Uhispania.

Kampeni za mchujo wa kufuzu kwa fainali za AFCON 2021 na fainali za Kombe la Dunia mnamo 2022 zikikaribia, timu za taifa zilizoagana na wakufunzi wao mwishoni mwa fainali za AFCON 2019 zimeanza pia kujisuka upya.

Misri walioagana na kocha Javier Aguirre mnamo Julai wamemwajiri mwanasoka wao wa zamani, Hossam El Badry, 59. Misri wamepangwa na Kenya, Togo na Como- ros katika Kundi G la kufuzu kwa AFCON 2021. Cameroon ambao watakuwa wenyeji wa fainali hizo, wamempokeza mikoba mwanasoka wa zamani wa Ureno, Toni Conceicao mikoba ya timu yao ya taifa almaarufu Indomitable Lions.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 57 amewahi pia kuwania vijana wa CFR Cluj nchini Romania.

Uteuzi wake ulichochewa na ulazima wa Indomitable Lions kulijaza pengo la kocha Clarence Seedorf aliyefurushwa Julai.