Mkufunzi wa Senegal pabaya, huenda akaadhibiwa kwa vurugu fainali ya AFCON2025
RABAT, MOROCCO
KOCHA wa Senegal Pape Thiaw huenda asisimamie timu hiyo kwenye mechi za Kombe la Dunia, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likitarajiwa kumwangushia adhabu kali kutokana na yaliyojiri kwenye fainali ya Kombe la Afrika (AFCON 2025) Jumapili.
Ripoti zinaarifu kuwa CAF imeudhika na tabia aliyodhihirisha Thiaw ambapo aliwaamrisha wachezaji waondoke uwanjani baada ya Morocco kupewa penalti ndani ya dakika za nyongeza baada ya muda wa kawaida wa kipindi cha kwanza kukamilika.
Thiaw hakufurahishwa na hatua ya Refa raia wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuwapa Morocco penalti dakika hizo za jioni.
Kocha huyo aliwaondoa wachezaji wake uwanjani akisema penalti hiyo haikuwa haki. Hata hivyo, walirejea uwanjani baada ya kushawishiwa na Mane.
Mvamizi Brahim Diaz alikosa penalti hiyo na Senegal ikashinda 1-0 muda wa ziada.
“CAF inalaani matukio yasiyozingatia maadili na kanuni za soka hasa yale yaliyolenga marefa na waandalizi wa mechi,” ikasema CAF kupitia taarifa.
“Pia CAF inaangalia video zote na suala hilo litashughulikiwa na kamati husika. Adhabu itahusisha faini na kupigwa marufuku kwa walioshiriki tabia zisizozingatia maadili,” ikaongeza taarifa ya CAF.
Senegal wamefuzu Kombe la Dunia ambalo litaandaliwa kuanzia June 11 hadi Julai 19 Amerika, Canada na Mexico.