MOKAYA: Alexis Sanchez ni mzigo kwa Man United, hana maana
Na JOB MOKOYA
TANGU Alexis Sanchez ajiunge na Manchester United, mambo yameenda mrama. Timu imekuwa ikang’ang’ana kupata ushindi ambao hauji kwa urahisi. Wakati mwingine ushinde.
Kwenye mechi nne za kwanza na Manchester United tangu Sanchez aingie, Manchester United ilipoteza mbili, moja ikiwa dhidi ya Tottenham na nyingine ikiwa dhidi ya Newcastle United. Kwenye mechi hizo zote, Sanchez alicheza.
Ujio wa Sanchez ingawa awali ulifurahiwa sana na mashabiki wengi wa United, sasa unadhihirika kuwa ambao haukufaa kitu. Labda angaliachwa tu aelekee Manchester City.
Matatizo ni mengi yanayoambatana na sajili huyu. Mosi, ni tatizo lake yeye mwenyewe. Sanchez anataka kufunga magoli. Na anataka kufunga magoli kwa lazima. Hivyo, atakimbiza mpira popote, kokote atafute bao. Matokeo yake ni kukosekana kufuatwa kwa mfumo mzuri wa uchezaji.
Martial na Rashford
Pili, ni swala la Martial na Rashford. Wakati Sanchez hakuwapo, ilikuwa lazima kwamba aidha Rashford au Martial wangecheza. Mmoja angeanza huku mwingine akiingia kipindi cha pili.
Na ushindani huu uliwafanya chipukizi hawa kung’ang’ania nafasi timu kwa kuonesha mchezo mzuri.
Kutokana na hayo, vijana hawa walionesha mchezo ulioenda skuli ukapata stashahada wakijua kwamba afanyaye masihara angalijipata benchini.
Ila sasa hali imebadilika. Weni wanajua kwamba Sanchez amechukua nafasi ya mmoja wao. Nyoyo zao zimekufa.
Hawachezi kwa kujituma. Martial hawatesi tena madifenda pale pembeni. Rashford hata haijulikani kama yuko timuni.
Hali ikiendelea hivi, kufikia mwishoni mwa msimu, naona mmojawapo wa chipukizi hawa akigura Manchester. Hata Mata vilevile anaweza akagura mji na kujaribu bahati kwingine.
Pogba
Tatu ni swala la Pogba. Sanchez anapocheza mwanzo huanzia pembeni mwa uwanja. Kama winga.
Ila, mara kwa mara atakimbia na kuchukua nafasi ya katikati ambayo kwa kawaida ni nafasi ya Pogba. Hilo humlazimu Pogba kurejea nyuma zaidi.
Hili ndilo lilomfanya Pogba kuondolewa na kuwekwa kwenye mechi dhidi ya Newcastle United. Aidha, alianza kwenye benchi kwenye mechi ya kombe la Carabao.
Kuna habari zinazoibuka kutoka Uhispania kwamba mibabe wa La Liga Real Madrid sasa inataka kumsajili Pogba msimu ujao kwa kima cha Pauni milioni 130.
Wendani wa karibu wa Pogba wanasema kwamba Pogba yuko tayari kuondoka Old Trafford baada ya mtu anayemzidi kwa mshahara kujiunga na timu. Kabla ya hapo, ni Pogba aliyepokea mshahara mkubwa zaidi katika ligi kuu ya Uingereza.
Aidha, habari hizo zinadai kwamba Pogba sasa hivi ametofautiana na meneja wake Jose Mourinho kuhusu mfumo wa uchezaji.
Tofauti hiyo huenda ikaenea na hata kuathiri wachezaji wengine timuni.
Tofauti kama hizi ndizo zilizomfanya Mourinho kuondoka Real Madrid pamoja na Chelsea, misimu miwili iliyopita.
Mourinho asipokuwa makini basi huenda akajipata akiguru Manchester Unied mwishoni mwa msimu