Michezo

MOKAYA: Solskjaer huenda akatimuliwa Manchester United ikilemewa na Liverpool

October 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOB MOKAYA

TIMU ya Manchester United inatarajia kumfuta kazi kocha wake Ole Gunnar Solskjaer wiki ijayo endapo itashindwa na Liverpool huku uongozi wa timu hiyo ukiwa umempa mechi mbili tu kabla ya kufanya uamuzi.

United imeshinda mechi mbili pekee za ligi kuu msimu huu na walipigwa na Newcastle United bao moja kwa bila juma lililopita kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa.

United iko katika nambari ya 12 kwenye jedwali la ligi kuu ya Uingereza.

Jumapili ijayo ndiyo inaweza kuwa siku ya mwisho kwa Solskjaer katika uga wa Old Trafford kama atapoteza mechi hiyo dhidi ya Liverpool. Kufutwa kazi kwa Solskjaer sasa ni suala la siku gani wala si iwapo huku akiwa amepewa mechi mbili tu kujiokoa. Mechi hizo ni dhidi ya Liverpool na Norwich.

Kwa mujibu wa ripoti za kuaminika, wamiliki wa United wamekubali kuwa United huenda ikashindwa na Liverpool lakini ushinde wa aina yoyote dhidi ya Norwish utakuwa ndio mwisho wa Solskajaer. Hata hivyo, ushinde dhidi ya Liverpool pia unaweza kuwa mwisho wake kutegemea idadi ya mabao.

Ikumbukwe kwamba kocha wa zamani wa Manchester United Jose Mourinho alipigwa kalamu mwezi Disemba mwaka jana baada ya United kupigwa mabao 3 kwa 1 na Liverpool. Ushinde kama huo utatosha pia kumtimua Solskjaer.

Kosa kubwa alilofanya kocha Solskjaer lilikuwa kuharakisha kuwauza washambulizi wake akianza na Romelu Lukaku na kisha Alexis Sanchez huku akidhani kuwa Marcus Rashford na Anthony Martial wangekuwa dawa mjarabu katika ushambulizi wa timu.

Kabla ya kuondoka kwa Mourinho, majarida mengi ya soka Uingereza yalichapisha habari zilizodai kwamba Mourinho alikuwa akimharibu Rashford kwa kutomchezesha na kumtegemea Lukaku.

Majarida hayo hata yalidai kwamba Rashford ndiye alikuwa mshambulizi bora kumshinda mchezaji yeyote Mwingereza na labda hata kumkaribia Messi na Ronaldo. Baada ya Lukaku na Sanchez kuondoka, imedhihirika kuwa Rashford hajui kitu.

Kwa shabiki yeyote wa Manchester United, mchezo wa Manchester United si wa kuridhisha na mashabiki wengi wameacha kutazama na kusubiri matokeo ambayo aghalabu huwa mabovu. Aidha, wanasubiri habari za kutimuliwa kwa limbukeni huyu asiye na mwao wa mpira.

Allegri

Hivi sasa mchakato wa kumtafuta kocha atakayemrithi Solskjaer unaendelea huku kocha wa zamani wa Paris Saint Germaine, PSG, Masimilliano Allegri akiongoza orodha ya makocha wanaopigiwa upato kupewa kazi hiyo.

Kocha mwingine ambaye anatarajia kufutwa ni kocha wa Tottenham Hostpurs Mauricio Pochetino ambaye ameandikisha msururu wa matokeo mabovu pamoja na kichapo cha mabao 7-2 dhidi ya Bayern Munich katika ngarambe ya Klabu Bingwa Ulaya.

Vile vile, United inavizia pembeni Pochettino apigwe kalamu ili kumkabidhi mikoba ya kuiongoza baada ya kumtimua Solskjaer.

Pochettino anapitia hali ngumu sana na mashabiki wengi kutoka Kenya wanaamini kwamba hali hiyo inatokana na kiungo mkabaji Victor Wanyama kutochezeshwa na hivyo safu ya kati inakuwa na wakati mgumu kukabili timu pinzani.