Michezo

Montreal Impact anayochezea Wanyama yakataa kufichua visa vya corona kambini mwake

June 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Montreal Impact haina mpango wowote wa kuzungumzia visa vya maambukizi ya virusi hatari vya corona katika kambi yake.

Impact, ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS), imeajiri kiungo Victor Mugubi Wanyama, ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars.

Vyombo vya habari nchini Canada inakotoka Impact vimeripoti kuwa wachezaji 18 na maafisa sita kutoka orodha ya 668 walipimwa kutoka klabu za MLS, wamepatikana na virusi hivyo tangu zirejelee mazoezi Juni 4. Hata hivyo, vyombo hivyo havijafanikiwa kupata majina ya wagonjwa hao.

Hapo Juni 29, msemaji wa klabu ya Impact alisisitiza kuwa klabu hiyo haitafichua kisa chochote katika kambi yake.

Hata hivyo, msemaji huyo alirejelea kuwa tangu timu hiyo irejee mazoezini uwanjani Nutrilait Center, wachezaji na maafisa wote wamekuwa wakipimwa kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa mara tu wanapofika kufanya mazoezi.

Klabu zote 26 za MLS zinatarajiwa kudumisha usafi zinapojiandaa kushiriki mashindano ya MLS is Back mjini Orlando katika jimbo la Florida kutoka Julai 8 hadi Agosti 11. Impact, ambayo inanolewa na nyota wa zamani wa Arsenal na Ufaransa Thierry Henry, itasafiri Julai 2 kilomita 2,305 hadi Orlando.

Juma lililopita, kituo kimoja cha redio kiliripoti kuweko visa viwili vya maambukizi ya ugonjwa wa covid-9 katika kikosi cha Henry vilivyosababisha shughuli ya mazoezi ya Jumanne na Jumatano kufutiliwa mbali.

Hata hivyo, habari hizo zilisemekana kuwa zisizo kweli baada ya wachezaji wote kuonekana mazoezini.

Impact itajibwaga uwanjani dhidi ya New England Revolution mnamo Julai 9 kwa mechi yake ya kwanza ya Kundi C. Mechi zake zingine za makundi zitasakatwa Julai 15 dhidi ya mahasimu wa tangu jadi Toronto kabla ya kukamilisha mechi za Kundi C dhidi ya DC United mnamo Julai 21.

Mechi ya kufungua mashindano hayo itakutanisha Inter Miami inayomilikiwa na nyota Muingereza David Beckham, dhidi ya Orlando City mnamo Julai 8.

Inter Miami, Orlando City, New York City, Philadelphia Union, Chicago Fire na Nashville SC ziko katika Kundi A.

Kundi B linajumuisha Seattle Sounders, FC Dallas, Vancouver Whitecaps na San Jose Earthquakes. Real Salt Lake, Sporting Kansas City, Colorado Rapids na Minnesota United zinaunda Kundi D, huku Atlanta United, FC Cincinnati, New York Red Bulls na Columbus Crew zikikutanishwa katika Kundi E.

Los Angeles FC, LA Galaxy, Houston Dynamo na Portland Timbers zinakamilisha orodha ya timu zitakazoshiriki mashindano haya ya timu za Amerika na Canada.