Michezo

Montreal Impact yapokea kichapo chake cha tatu mfululizo

September 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Montreal Impact ilipokea kichapo chake cha tatu mfululizo na cha nane katika mechi 12 zilizopita baada ya kutitigwa 3-1 dhidi ya New England Revolution kwenye Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS) mapema leo Alhamisi.

Nahodha wa Harambee Stars Victor Wanyama amecheza dakika zote 90 katika michuano hiyo. Dhidi ya New England hapo Septemba 24, raia wa Finland Lassi Lappalainen alifungia Montreal bao la kufutia machozi dakika ya 86.

Montreal, ambayo inanolewa na Mfaransa Thierry Henry, ilizamishwa na mabao kutoka kwa beki Henry Kessler dakika ya 45, raia wa Argentina Gustavo Bou na mshambuliaji wa Uruguay Diego Fagundez.

Vijana wa Henry watakutana na klabu yake ya zamani New York Red Bulls katika mechi ijayo mnamo Septemba 28. Montreal inashikilia nafasi ya nane kwa alama 16 baada ya kusakata mechi 13 kwenye ligi ya ukanda wa Mashariki. Bulls iko alama moja mbele katika nafasi ya saba.

Mapema leo Alhamisi, kiungo mshambuliaji Cliff Nyakeya kutoka Kenya alichezeshwa mechi nzima na klabu yake ya Masr ikipoteza 3-0 dhidi ya miamba Al Ahly kwenye Ligi Kuu ya Misri.

Amr Soleya alifunga penalti dakika ya saba nao Kahraba na raia wa Nigeria Junior Ajayi wakaongeza mabao katika kipindi cha pili. Masr ilipoteza penalti mapema katika kipindi cha pili iliyopigwa na Mostafa Soltan.

Nchini Uingereza, Barnsley anayochezea beki Clarke Oduor ilibanduliwa kwenye kipute cha League Cup (Carabao) kwa kuaibishwa 6-0 na vijana wa Frank Lampard, Chelsea 6-0 uwanjani Stamford Bridge mnamo Jumatano usiku.

Oduor aliingia uwanjani dakika ya 57 kama mchezaji wa akiba, tayari Barnsley ikiwa imefungwa mabao manne kupitia kwa Tammy Abraham (dakika ya 19), Kai Havertz (28 na 55) na Ross Barkley (49).

Mjerumani Havertz aliongeza bao la tano dakika ya 65 kabla ya Mfaransa Olivier Giroud kukamilisha maangamizi hayo dakika ya 83. Barnsley inashiriki Ligi ya Daraja ya Pili baada ya kuponea pembamba kuangukiwa na shoka ilipoduwaza Brentford 2-1 katika mechi ya kufunga msimu 2019-2020 Oduor akiifungia bao la ushindi.