Michezo

Moraa aambulia shaba ya 800m Olimpiki  

Na GEOFFREY ANENE August 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BINGWA wa dunia mbio za mita 800, Mary Moraa ameridhika na medali ya shaba kwenye Michezo ya Olimpiki baada ya kumaliza mizunguko hiyo miwili katika nafasi ya tatu kwa dakika 1:57.42 mjini Paris nchini Ufaransa, Jumatatu, Agosti 5, 2024.

Moraa, ambaye alibanduliwa katika nusu-fainali katika makala ya 2020 mjini Tokyo, Japan mwaka 2021, alijaribu kufyatuka baada ya kupiga kona ya mwisho, lakini bila mafanikio.

Muingereza Keely Hodgkinson, ambaye alipata nishani ya fedha mjini Tokyo, alitwaa dhahabu kwa 1:56.72, huku fedha ikimwendea Muethiopia Tsige Duguma (1:57.15).

Moraa, ambaye ni bingwa wa Jumuiya ya Madola na alikuwa Mkenya pekee katika fainali Jumatatu, Agosti 5, 2024 baada ya Vivian Kiprotich na Lilian Odira kubanduliwa katika nusu-fainali, ni Mkenya wa tatu tu kupata medali katika 800m kwenye Olimpiki tangu mbio hizo zijumuishwe mashindanoni mwaka 1928.

Pamela Jelimo alinyakua dhahabu mwaka 2008 mjini Beijing, Uchina na kisha shaba mwaka 2012 mjini Londo, Uingereza.

Margaret Wambui aliambulia shaba katika makala ya 2016 mjini Rio de Janairo, Brazil.

Baada ya medali hizo mbili, Kenya sasa ni nambari 34 duniani kwa dhahabu moja na shaba moja kutoka orodha ya zaidi ya mataifa 200 yanayoshiriki.