Moraa ashindia Kenya dhahabu ya tatu Riadha za Afrika
Na GEOFFREY ANENE
Mary Moraa amepeperusha bendera ya Kenya vilivyo katika siku ya pili ya Riadha za Afrika za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 na 20 jijini Abidjan nchini Ivory Coast, Jumatano.
Moraa ametesa wapinzani wake katika mbio za mita 400 akikamilisha mzunguko huo mmoja kwa sekunde 53.55.
Hapo Aprili 16, Kenya ilianza mashindano haya kwa kunyakua dhahabu kupitia kwa Bravin Kipkosgei na Vincent Kibet katika mbio za mita 10,000 na mita 1,500 mtawalia.
Kipkosgei aliongoza Mkenya mwenzake Emmanuel Korir kushinda medali ya dhahabu na shaba katika kitengo hicho cha mizunguko 25.
Kenya sasa ina jumla ya medali saba baada ya Kibet kuongoza Peter Kibui kuvuna dhahabu na shaba mtawalia katika mbio za mita 1,500 za wakimbiaji wasiozidi umri wa miaka 18.
Janet Nyiva na Emmaculate Akinyi walishindia Kenya nishani za fedha katika mbio za mita 1,500 na mita 3,000 katika mashindano ya Under-18 na Under-20 mtawalia.
Keter alikamilisha mbio za mita 1,500 kwa dakika 3:40.28 akifuatwa na Muethiopia Fentahun Gezahignyihun (3:43.64) naye Kibui akafunga tatu-bora kwa 3:45.50. Nyiva alimaliza mita 1,500 za Under-18 kwa dakika 4:20.43.
Mmoroko Meryem Azrour alinyakua dhahabu kwa dakika 4:20.14 naye Muethiopia Girma Tilahunalmaz akaridhika na shaba (4:21.97). Mkenya Maureen Cherotich alikamilisha katika nafasi ya nne (4:24.09).