• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
Morata alishwa kadi ya manjano na mpenziwe, onyo atabaki mseja

Morata alishwa kadi ya manjano na mpenziwe, onyo atabaki mseja

Na MASHIRIKA

KIDOSHO Alice Campello ambaye ni mkewe fowadi matata wa Chelsea na timu ya taifa ya Uhispania, Alvaro Morata ametishia kumrejesha mwanasoka huyo katika ukapera wa lazima iwapo hatadumisha nidhamu yake akiwa ugani.

Kwa mujibu wa Alice ambaye alimzalia Morata mtoto wa kiume mwishoni mwa Aprili, yeye huudhika sana kila mara mumewe anapoadhibiwa na marefa kwa makosa ambayo nyota huyo angeepuka.

Tangu makali ya Morata, 25, yashuke pakubwa uwanjani, kocha Antonio Conte amepania kumwajibisha sana Olivier Giroud badala ya mvamizi huyo wa zamani wa Real Madrid.

Hofu kubwa ya Alice ni kwamba huenda mumewe akakosekana kabisa katika mipango ya baadaye ya Chelsea iwapo atashindwa kuzidhibiti hisia na hasira zake kila anapoonywa na marefa.

Kufikia sasa, Morata amelishwa jumla ya kadi 10 za manjano na moja nyekundu, jambo ambalo Alice amesema litamchochea kutafuta hifadhi ya mapenzi yake kwingineko.

Mnamo Februari 2018, Alice alionya kwamba atakuwa mwepesi wa kumtema Morata iwapo nyota huyo atapoteza mkwaju wowote wa penalti kwenye kampeni za EPL katika msimu wa 2017-18.

Alice alilitoa tishio hilo baada ya Watford kuwatafuna Chelsea kama Big-G uwanjani Vicarage Road mnamo Februari 5, miezi michache baada ya Morata kupoteza penalti dhidi ya Arsenal.

Alice ambaye ni mwanamitindo mzawa wa Italia, alijitosa katika mtandao wake wa Instagram kwa mara ya kwanza wiki jana na kubainisha furaha ya kuitwa mama baada ya kujifungua mtoto wao wa kwanza.

Morata alimfanya Alice kuwa wake wa halali mnamo Juni 2017 kwenye sherehe za harusi zilizoandaliwa katika ukumbi wa Basilica del Redentore jijini Venice, Italia.

Kabla ya kufunga silisili za maisha na Alice ambaye pia ni gwiji wa fasheni za mavazi ya kike, Morata alikuwa akitoka kipamzi na Maria Pombo, kipusa aliyechumbiana naye kwa miaka miwili kabla ya jicho lake kumwona Alice mwanzoni mwa 2015.

 

You can share this post!

Jombi aumia mazishini aking’ang’ania chakula

Trump aisifu Korea Kaskazini kwa kuharibu kituo cha nyuklia

adminleo