Michezo

Motisha baada ya KWPL kutengewa Sh14 bilioni

July 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

KOCHA wa timu ya Eldoret Falcons, Joshua Ariko analitaka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) liwazie upya kuhusu ngarambe ya Ligi Kuu ya Soka la Wanawake(KWPL). 

Aidha anashukuru serikali kwa kuteingea sekta ya michezo Sh14 bilioni katika bajeti ya kitaifa ya mwaka wa 2020-21 ambapo endapo zitatumiwa vizuri zitaimarisha makuzi ya fani mbali mbali nchini.

Katika bajeti ya mwaka huu, Wizara ya Michezo, Sanna na Utamadumi ilitengewa fedha hizo kinyume na mwaka uliyopita ilipotengewa Sh5.3 bilioni.

PICHA HALISI

Hii inamaanisha ipo nyongeza ya Sh8.7 bilioni mwaka huu, fedha ambazo wadau wengi walisema zitapaisha pakubwa mashirikisho ya spoti ambayo tayari yamewasilisha bajeti zao kwa minajili ya kampeni za msimu ujao.

”FKF haina budi kuzungumza na Wizara ya Michezo angalau ipate fedha za kugharamia mahitaji muhimu ili kuhakikisha mechi za kipute hicho zitachezwa kama ligi moja badala ya kuzigawanya mara mbili,” alisema na kuongeza kwamba hatua hiyo itasaidia pakubwa kuboresha kiwango cha mchezo huo.

Anadokeza kuwa mpango wa kugawanya michezo ya ngarambe hiyo mara mbili, Kundi A na B hutautaonyesha picha halisi ya kiwango cha mchezo huo kwa wanawake.

”Kiukweli mpango huo hautafanikisha utaratibu wa kuteua wachezaji wa timu ya Harambee Starlets. Itakuwa vigumu kwa kocha mkuu kuteua wachezaji wale bora.”

VIKOSI 16

”Katika Ligi ya KWPL inayojumuisha timu 16 tunahitaji zote zipatane ili kutambua gani bora pia ni wachezaji wepi wakali kuliko wengine. Itakuwa vizuri endapo uongozi wa sasa utajadili suala hilo na Wizara ya Michezo angalau kutafuta namna ya kufadhili kipute hicho.”

Anasema kulingana na ratiba iliyotolewa mapema mwaka huu kabla ya kutokea kwa mlipuko wa corona ni wazi timu za Magharibi mwa Kenya hasiwezi kucheza dhidi ya wenzao katika Kaunti ya Nairobi ambao wamepangwa Kundi A.

Pendekezo lake linaungwa mkono na kocha, wa Ulinzi Starlets, Joseph Wambua Mwanza iliyopandishwa ngazi mapema muhula huu.

”Ili kupima wachezaji wangu tunahitaji kucheza dhidi ya kila timu inayoshiriki mechi za kinyangányiro cha msimu huu” Wambua alisema na kuomba uongozi wa FKF kuwazia upya suala la kufanya ligi hiyo kuwa moja.

Kadhalika alidokeza mechi za ligi moja zitatoa ushindani wa kweli na kupima uwezo wa wachezaji wote.

MAKUNDI

Kulingana na ratiba ya kipute hicho Kundi A linashirikisha: Thika Queens, Gaspo Women, Kayole Starlets, Zetech Sparks, Ulinzi Starlets, Makolanders, Kibera Girls Soccer Academy (KGSA) na Mathare United Women (MUW FC). Nalo Kundi B linajumuisha: Vihiga Queens, Eldoret Falcons, Trans Nzoia Falcons, SEP Oyugis, Oserian Ladies, Wadadia LG, Kisumu Allstarlets na Nakuru West Queens.