• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
MOTO SANA: Arsenal moto kwa Valencia, yatinga fainali ligi ya Uropa

MOTO SANA: Arsenal moto kwa Valencia, yatinga fainali ligi ya Uropa

Na MASHIRIKA

VALENCIA, Uhispania

ARSENAL ilidhihirisha ni ‘moto wa kuotea mbali’ kwenye soka ya Bara Ulaya msimu huu baada ya kutitiga Valencia 4-2 katika Ligi ya Uropa kwa jumla ya mabao 7-3 Alhamisi na kujikatia tiketi ya kukutana na Chelsea katika fainali jijini Baku mnamo Mei 29.

Vijana wa Unai Emery, ambao wamekuwa na rekodi isiyotamanika kwenye Ligi Kuu ya Uingereza ugenini msimu huu, walizidi kutesa katika ardhi ya wenyewe kwenye Ligi ya Uropa baada ya kuzamisha Valencia kupitia kwa mabao ya Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette katika nusu-fainali uwanjani Mestalla.

Chelsea walilemea Eintracht Frankfurt kutoka Ujerumani kwa penalti 4-3 baada ya mikondo yote miwili kutamatika 2-2 uwanjani Stamford Bridge.

Ushindi wa Arsenal na Chelsea ulitimia siku moja tu baada ya timu zingine mbili za Uingereza Tottenham na Liverpool kutinga fainali ya Klabu Bingwa.

Hapo Alhamisi, raia wa Gabon, Aubameyang alikuwa mwiba kwa Valencia baada ya kuimiminia mabao matatu. Lacazette alichangia bao moja. Wenyeji Valencia walikuwa wamelimwa 3-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza uwanjani Emirates. Jinsi walivyoanza mechi ya mkondo wa kwanza kwa kufungua ukurasa wa magoli ndivyo ilivyokuwa katika mechi ya marudiano pale Kevin Gameiro alipotikisa nyavu dakika ya 11.

Hata hivyo, Arsenal, ambayo inategemea kushinda kombe hili kuingia Klabu Bingwa Ulaya msimu 2019-2020, ilijibu dakika sita baadaye kupitia kwa Aubameyang na kuenda mapumzikoni zikiwa 1-1.

Emery, ambaye alishinda Ligi ya Uropa mwaka 2014, 2015 na 2016 akinoa Sevilla nchini Uhispania, kisha alishuhudia vijana wake wakichukua uongozi 2-1 dakika tano baada ya kipindi cha pili kuanza kupitia kwa Lacazette. Hata hivyo, Gameiro, ambaye alishinda Ligi ya Uropa mara nne akichezea Sevilla na Atletico Madrid, alisawazisha 2-2 dakika ya 58. Aubameyang kisha alirejesha Arsenal kifua mbele 3-2 dakika ya 69 kabla ya kuzamisha chombo cha Valencia kabisa zikisalia dakika mbili muda wa kawaida utamatike.

Ushindi huu unarejesha Arsenal nchini Azerbaijan kwa fainali. Ilichabanga miamba wa Azerbaijan, Qarabag 3-0 mapema katika kampeni yake ya Ligi ya Uropa mwezi Oktoba 2018. Ni mara ya kwanza tangu Tottenham ichape Wolves katika fainali ya makala ya kwanza kombe hili likiitwa Uefa Cup mwaka 1972 fainali ya mashindano haya ya daraja ya pili itahusisha timu zote kutoka nchini Uingereza.

Chelsea ilijikatia tiketi baada ya kufungiwa penalti zake na Ross Barkley, Jorginho, David Luiz na Eden Hazard. Eintracht iliongoza upigaji wa penalti 2-1 baada ya Sebastien Haller na Luka Jovic kumwaga kipa Kepa Arrizabalaga.

Hata hivyo, baada ya penalti ya Cesar Azpilicueta kupanguliwa na Kevin Trapp, Eintracht ilifanikiwa kufuma wavuni penalti moja tu kupitia kwa Jonathan de Guzman, huku Kepa akiwazima Martin Hinteregger na Goncalo Paciencia.

Arsenal itakuwa ikishiriki fainali yake ya pili ya Ligi ya Uropa baada ya kubwagwa na Galatasaray kutoka Uturuki mwaka 2000.

Chelsea ya kocha Maurizio Sarri ilishinda taji hili mwaka 2013 ilipokung’uta Benfica ya Ureno.

  • Tags

You can share this post!

Vikwazo katika biashara ya nyama vyawekwa eneo la Kati

Clarence Mwangi: Kutoka shamba boi hadi mmiliki wa kampuni

adminleo