MOU AWAKA! Spurs yafinywa 3-2 na Norwich
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
KOCHA Jose Mourinho alimkemea vikali mchezaji wake, Eric Dier baada ya kiungo huyo kumrukia shabiki aliyemtusi Tottenham Hotspur ilipobanduliwa nje ya Kombe la FA, Jumatano usiku.
Hata hivyo, Mourinho ameomba Spurs isimchukulie Dier hatua zozote za kinidhamu licha ya kumsuta kiungo huyo.
Spurs walifinywa 3-2 na Norwich kwa njia ya penalti, na sarakasi zilizozuka kwenye mechi hiyo zilimshuhudia Dier akiruka sehemu ya chini ya mashabiki na kumkabili mwanamume huyo anayedaiwa kumtusi.
Video ya tukio hilo imeenea kwenye mitandao ya kijamii huku Mwingereza huyo akitarajiwa kuadhibiwa kwa kukiuka sheria za Shirikisho la Soka nchini Uingereza (FA) na pia Tottenham.
“Nadhani Eric Dier alifanya kitu ambacho sisi kama wataalamu hatuwezi kufanya, lakini katika hali kama ile tunajipata tukisukumwa kufanya,” alisema Mourinho.
“Kwa sababu mtu anapokutusi na familia yako iko hapo, halafu umekabili nadhani Eric alikosa ustaarabu. Mtu huyo alitusi Eric familia yake ikiwa hapo. Ndugu yake mdogo hakufurahia hilo na hapo ndipo Eric, narudia tena kwamba alichokifanya si kile wataalamu wanastahili kufanya, lakini alichukua hatua ambayo pengine wengine wetu tungechukua.”
Tukio hilo lilifanyika karibu na eneo la wachezaji kuingia uwanjani, ambalo mashabiki huwa ni wa mashirika, huku Mourinho akiwakosoa kwa kutokuwa “mashabiki wa kweli wa Tottenham.”
“Watu hao wanashikilia vyeo vya juu,” aliongeza Mreno huyo. “Bila shaka, baadhi yao ni mashabiki wa Tottenham, lakini nadhani wengi wao wamealikwa tu. Wanaketi katika sehemu ya uwanja ambayo mara nyingi mimi huwa na tashwishi kama wao ni mashabiki wa Tottenham.”
Matokeo ya mchuano huo ni pigo jingine kwa Spurs kwa sababu inachechemea katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Kwenye mechi hiyo ya raundi ya tano, Jan Vertonghen alipatia Spurs uongozi katika dakika ya 13. Lakini Josip Drmic alisawazishia Norwich dakika ya 78 baada ya kipa Michel Vorm kufanya masihara michumani.
Hakuna aliyeona lango tena katika muda wa kawaida na pia katika dakika 30 za ziada. Hivyo, mechi ililazimika kuingia katika mikwaju ya penalti ili kuamua mshindi.
Kipa wa Norwich, Tim Krul ndiye alikuwa shujaa wa mechi alipopangua penalti mbili za Tottenham zake Troy Parrott na Gedson Fernandes. Dier alionekana akimtuliza Fernandes uwanjani kabla ya kuelekea eneo la mashabiki kuzua fujo.