Michezo

Moukoko sasa ndiye mchezaji wa umri mdogo zaidi kuwahi kufunga bao katika historia ya soka ya Bundesliga

December 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

YOUSSOUFA Moukoko wa Borussia Dortmund aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kufunga bao katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) licha ya waajiri wake kupepetwa 2-1 na Union Berlin mnamo Jumamosi.

Akiwa na umri wa miaka 16 na siku 28 pekee, Moukoko, alisawazishia Dortmund katika dakika ya 60 baada ya Taiwo Awoniyi kuwaweka Union kifua mbele katika dakika ya 57. Bao la ushindi kwa upande wa Union lilipachikwa wavuni na Marvin Friedrich.

Kwa kutikisa nyavu za wenyeji wao, Moukoko aliipiku rekodi ya zamani ya Florian Wirtz aliyefungia Bayer Leverkusen dhidi ya Bayern Munich akiwa na umri wa miaka 17 na siku 34 pekee mnamo Mei 2020.

Dortmund waliomfuta kazi kocha Lucien Favre mnamo Disemba 13 baada ya kupokezwa kichapo cha 5-1 kutoka kwa Stuttgart kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne jedwalini kwa alama 22, moja mbele ya nambari tano Union.

Moukoko ambaye ni mzawa wa Cameroon sasa ni raia wa Ujerumani ambao humtegemea katika kikosi chao cha chipukizi wa U-20. Aliweka rekodi nyingine mapema msimu huu kwa kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuchezeshwa katika Bundesliga alipoingia uwanjani dhidi ya Hertha Berlin mnamo Novemba 22, siku moja baada ya kutimu umri wa miaka 16.

Baadaye, Moukoko aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mchanga zaidi kuwahi kuwajibishwa katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) alipowaongoza Dortmund kucharaza Zenit St Petersburg mnamo Disemba 9, 2020.